Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi (aliyenyanua ubao) akipiga ubao wa kuashiria
uzinduzi wa michezo ya UMISSETA mkoa wa Singida, mbele yake ni wanariadha
wakianza mashindano.
Wanamichezo kutoka
Shule za Sekondari za Halmashauri ya wilaya ya Itigi wakiimba wimbo wa taifa
kabla ya kuanza mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi (katikati) akiimba wimbo wa taifa kabla ya kuanza
mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa, kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi na Kulia Kwake ni Afisa Elimu Mkoa wa
Singida Florian Kimolo.
Halmashauri zote saba
za Mkoa wa Singida zimeagizwa kutenga maeneo yenye hadhi ya kuwa viwanja vya
michezo pamoja na kuhakikisha zinakuwa na benki ya wanamichezo katika
halmashauri zao.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa maagizo hayo leo asubuhi kabla ya kuzindua
mashindano ya michezo kwa shule za Sekondari (UMISSETA) kwa ngazi ya mkoa
ambapo wanamichezo hao wataunda timu za Mkoa kwa ajili ya mashindano ya kitaifa
yatakayofanyika jijini Mwanza mwezi ujao.
Dkt. Nchimbi amesema halmashauri
zimekuwa zikiwatelekeza wanamichezo mahiri hivyo wakianzisha benki ya
wanamichezo kwa maana ya kuhifadhi kumbukumbu za wana michezo mahiri pamoja na
kuwaendeleza hawatapata shida kipindi cha mashindano yoyote.
Ameongeza kuwa halmashauri
zimekuwa zikijisahau katika kuandaa maeneno ya michezo hadi inapofika kipindi
cha UMISETA hali inayopelekea kukosekana kwa viwanja vya kufanyia mazoezi ili
kuwa na timu bora.
Dkt. Nchimbi amewaasa
wana michezo kuwa na nidhamu, utii, bidii na kuitumia michezo kuutangaza Mkoa
wa Singida wenye fursa nyingi za uwekezaji pamoja na kujitangaza uwezo wao ili
waweze kupata nafasi katika timu mbalimbali za kitaifa.
Aidha amewasisitiza
waamuzi wa michezo kutenda haki kwakuwa matendo yao ni darasa la nidhamu na
maadili kwa wanafunzi wao na kuwatahadharisha wanafunzi wasio tii kuwa hawatapata
nafasi katika timu ya Mkoa.
Kwa upande wake
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt Angelina Mageni Lutambi amewapongeza
wakurugenzi wa halmashauri kwa kufanikisha upatikanaji na ushiriki wa timu za
michezo za kila halmashauri.
Dkt. Lutambi
ameishukuru pia kampuni ya Coca cola kwa udhamini wa UMISSETA kwa kutoa vifaa
kwa shule 118 ambavyo ni tisheti 3,776, mipira ya miguu 118 na mipira ya
basketball 118 pamoja na ahadi ya kuendelea kugawa vifaa katika shule 45
zilizobaki.
Ameongeza kwa
kuwasihi wana michezo wote kucheza kwa nidhamu ya hali ya juu, kwa kuzingatia sheria
na kanuni za michezo ili kutengeneza timu ya ushindi ya mkoa.
Akisoma taarifa ya
Michezo ya Umiseta Afisa Michezo wa Mkoa Henry Kapella amesema jumla ya wana
michezo 576 wameshiriki katika michezo hiyo ambapo wataunda timu ya mkoa ya
michezo ya bao, riadha, mpira wa miguu na mpira wa pete.
Kapella ameongeza
kuwa kauli mbiu ya michezo ya Umisseta kwa mwaka 2017 ni ‘Wekeza katika michezo
kwa ustawi wa elimu na Viwanda’.
Kwa upande wao wanafunzi
walioshiriki mashindano ya umisseta wamesema michezo inawajenga kiafya na
kiakili kwa kuwa wanafunzi wanaoshiriki katika michezo huwa na ufaulu mzuri wa
masomo yao.
Wameongeza kuwa
michezo inawaongezea nidhamu na kuwajenga kimaadili hivyo kufaulu inakuwa ni
rahisi, aidha wamesema michezo ina faida nyingi ikiwemo kuwatengenezea ajira
mara baada ya kumaliza masomo yao.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt. Rehema Nchimbi akihutubia kabla ya kuzindua mashindano ya UMISSETA
ngazi ya Mkoa wa Singida.
Katibu Tawala Mkoa wa
Singida Dkt. Angelina Mageni Lutambi akizungumza katika uzinduzi wa mashindano
ya UMISSETA Mkoa wa Singida.
No comments:
Post a Comment