Waziri
wa Mambo ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwigulu Nchemba akiwasha
gari la kubebea wagonjwa (ambulance), katika kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago
jimbo la Iramba.
Mkazi
wa kijiji cha Urughu jimbo la Iramba mkoani Singida Jumanne Hatibu akizungumza
kwenye hafla ya makabidhiano ya gari la kubebea wagonjwa lililotolewa na serikali
kupitia wizara ya afya jinsia, wazee na watoto.
Waziri
wa Mambo ya ndani na Mbunge wa jimbo la Iramba mkoani Singida Mwigulu Nchemba akizungumza
kwenye hafla ya kukabidhi gari la kubebea wagonjwa (ambulance) katika
kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago jimbo la Iramba.
Na Nathaniel Limu-Singida.
Waziri wa Mambo ya Ndani na
Mbunge wa jimbo la Iramba Mkoani Singida Mwingulu L. Nchemba, amekabidhi gari
la kubebea wagonjwa mpya na la kisasa ambalo limetolewa na serikali kupitia
Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kituo cha afya cha Ndago kilichopo
Wilayani Iramba.
Mwigulu ameagiza gari hilo
lisitumike kama taksi au gari la kubebea mkaa, bali litumike kwa kazi
iliyokusudiwa ambayo ni kubebea wagonjwa na akina mama wajawazito tu.
Mbunge huyo ameyasema hayo juzi
wakati akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi ‘ambulance’ hiyo iliyofanyika
katika kijiji cha Ndago jimbo la Iramba na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi.
Aidha, amesema ni marufuku wagonjwa
kuombwa kuchangia mafuta ya ambulance hiyo au gharama yo yote ile,
gari hili wagonjwa walitumie bure.
“Gari hilo lipatikane kituoni
wakati wote. Liwe na mafuta ya kutosha na dereva awepo. Gari hili ambalo ni la
kisasa, litunzwe na kulindwa ili liweze kutumika kwa miaka mingi ijayo”, alisema
Mwigulu.
Mbunge huyo ameishukuru serikali ya
awamu ya tano chini ya rais Magufuli na waziri Ummy kwa msaada huo ambao
utaokoa wapiga kura wake na wananchi kwa ujumla.
Awali mganga mfawidhi wa kituo
cha afya cha Ndago, Dkt Lyoce Mgelwa, alisema kituo hicho kinahudumia tarafa
nzima ya Ndago yenye wakazi 89,882.
Pia alisema kituo hicho kinapokea
wagonjwa wanaopata rufaa katoka kwenye zahanati 10 zilizopo katika tarafa ya
Ndago.
Dkt Lyoce alisema msaada huo wa
kupatiwa gari la kubeba wagonjwa ambulance, utapunguza kero zinazowakabili
wagonjwa wanaopewa rufaa kuchelewa kufika kwa wakati katika hospitali ya
wilaya.
“Wagonjwa wanaopewa rufaa watawahishwa hospitali
ya wilaya ili kuokoa maisha ya wagonjwa na hasa akina mama wajawazito na
watoto chini ya miaka mitano. Upunguzaji wa vifo hivyo, wilaya itakuwa imepiga
hatua kubwa kufikia lengo namba nne na tano la maendeleo ya milenia hadi kufika
mwaka 2020”, alisema.
Aidha, Dkt Locye ametumia fursa
hiyo kuomba wadau mbalimbali kuwaunga mkono katika kukamilisha jengo lao la
kulaza wagonjwa (wodi).
“Wananchi wa jimbo la Iramba,
tunaendelea kukushukuru wewe mbunge wetu Mwingulu kwa misaada mingi
unayoendelea kuitoa kwenye maeneo mbalimbali katika kuboresha huduma za jamii,
ikiwemo huduma muhimu za afya”, alisema.
Kwa upande wake Jumanne Hatibu
mkazi wa kijiji cha Urughu tarafa ya Ndago alisema kabla ya ujio wa ambulance
hiyo kijiji hicho kilikuwa kinakabiliwa na tatizo sugu la usafiri kwa wagonjwa
hasa akina mama wajawazito.
“Kijiji chetu kwa miaka mingi tulikuwa
tukitegemea usafiri wa basi na lilikuwepo basi moja tu. Likiondoka asubuhi
kwenda Singida hakuna tena usafiri kwa siku husika hadi kesho asubuhi. Kwa hiyo
kwa wagonjwa na hasa akina mama wajawazito, ilikuwa ni changamoto kubwa.
Ambulance hii, itaokoa maisha ya wakazi wa tarafa ya Ndago na maeneo jirani”, alisema
Hatibu ambaye ni mlemavu wa miguu.
Wakati huo huo, Mbunge Mwingulu ameahidi kuchangia ujenzi wa wodi ya kituo cha
afya Ndago kwa kutoa mifuko mia moja ya saruji.
No comments:
Post a Comment