Afisa Utumishi Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Justo Herman akikagua noti halali wakati wa mafunzo
yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.
Afisa Maendeleo ya
Jamii Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango na Afisa Elimu wa Mkoa wa Singida
Florian Kimoro wakionyeshana alama za noti halali wakati wa mafunzo yaliyotolewa
na Benki Kuu ya Tanzania.
Benki Kuu ya Tanzania (BOT) imetoa mafunzo kwa watumishi wote wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida juu ya alama zinazopatikana katika noti halali za fedha ya Tanzania leo asubuhi katika ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Akitoa mafunzo hayo Afisa
Kutoka Benki Kuu ya Tanzania Rehema Zongo amewafafanulia watumishi hao namna ya
kutambua noti halali kwa vitendo huku akisisitiza alama muhimu zinazopatikana
katika noti halali ili waweze kutofautisha na zile bandia.
Zongo amesema
watumishi wanatakiwa kuichunguza noti halali, waipapase ili kuhisi mparuzo
kwenye maneno yaliyoandikwa kwa maandishi maalumu mfano maandishi yanayoeleza
fedha halali kwa malipo ya shilingi mia tano, elfu moja, elfu mbili, elfu tano
na elfu kumi.
Amewasisitizia kuwa
wanaweza kuitambua noti halali kwa kuangalia sura ya Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere inayoonekana unapoimulika noti kwenye mwanga na pia kukagua utepe
maalumu kwenye noti za shilingi 500, 1000, 2000, 5000 na 10,000 unaoonekana
kama madirisha yenye umbo la almasi ambapo hubadilika badilika noti inapogeuzwa
geuzwa.
Zongo ameongeza kuwa
watumishi na wananchi wote wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kuwa noti bandia
zipo mtaani na kuwa hazina thamani yoyote.
“Ukipata noti bandia
au hata kama unaishuku ni bandia, ipeleke benki au kituo chochote cha polisi
kilichopo karibu nawe, lakini pia tuwe na utaratibu wa kuthibitisha uhalali wa
noti mara uzipatazo kwa kuzingatia alama tulizowafunzisha leo, na pia tunaomba
muwe waalimu kwa kuwafundisha wengine alama hizo”, amesema Zongo.
Amesisitiza kuwa
kugushi pamoja na kumiliki fedha bandia kwa nia ya kuzitumia ni kosa la jinai
linalosababisha mhusika kushitakiwa kwenye vyombo vya sheria hivyo wanapaswa
kuwa makini, kutoa taarifa sahihi na katika sehemu husika, pia kuwa na
utaratibu wa kuchunguza noti.
Kwa upande wake
Mhasibu Mkuu wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida George Kulwa kwa niaba ya
watumishi wote waliopata mafunzo hayo ameishukuru Benki kuu ya Tanzania kwa
kutoa mafunzo hayo.
George amesema elimu
iliyotolewa kwa watumishi hao ni muhimu na itawasaidia si watumishi wa ofisi ya
Mkuu wa Mkoa pekee bali wananchi wote kwa ujumla kwakuwa watumishi hao watakuwa
mabalozi wa elimu hiyo.
Aidha ameiomba benki
kuu kuendelea kutoa elimu hiyo mpaka ngazi za vijiji ili taifa lote liwe na
elimu sahihi na ya kutosha juu ya alama za noti halali huku akiwakaribisha tena
katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa kila mara wanapotaka kutoa elimu yoyote juu ya
masuala ya fedha na uchumi wa Tanzania.
Mwangalizi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida
Khadija Hamisi na Mkaguzi wa ndani Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida Alfred
Kalama wakisikiliza kwa umakini alama zinazopatika katika noti halali wakati wa
mafunzo yaliyotolewa na Benki Kuu ya Tanzania.
Mhasibu Mkuu wa Ofisi
ya Mkuu wa Mkoa wa Singida George Kulwa akitoa shukrani kwa niaba ya watumishi
wote waliopata mafunzo ya Benki kuu ya Tanzania.
Maafisa kutoka Benki
Kuu ya Tanzania Rehema Zongo na Rajab Ibrahimu wakisikiliza maswali na kutoa
ufafanuzi kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mara baada ya kutoa mafunzo ya
alama za noti halali.
Maafisa kutoka Benki
Kuu ya Tanzania Rehema Zongo na Rajab Ibrahimu wakisikiliza maswali na kutoa
ufafanuzi kwa watumishi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa mara baada ya kutoa mafunzo ya
alama za noti halali.
No comments:
Post a Comment