Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimkabidhi Diwani Viti maalum kata ya Ibaga Habiba Issa cheti cha mafunzo ya usimamizi wa miradi na jitihada za jamii za mbinu za kutambua fursa na vikwazo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akizungumza na madiwani kabla hajawapatia vyeti vya mafunzo ya usimamizi wa miradi na jitihada za jamii za mbinu za kutambua fursa na vikwazo.
Wanasiasa
wameshauriwa kuacha kuwakatisha tamaa wananchi kwa kuwaita masikini hali
inayosababisha washindwe kuchangia na kushiriki kikamilifu katika miradi na
shughuli za maendeleo hususani miradi ambayo ina ufadhili kidogo wa serikali na
wahisani.
Mkuu wa
Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi ametoa katazo hilo kabla ya kugawa vyeti
kwa waheshimiwa madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama waliofuzu mafunzo
kuhusu jitihada za jamii kupitia mbinu shirikishi ya fursa na vikwazo kwa
maendeleo iliyoboreshwa na usimamizi wa miradi ya maendeleo.
Dkt.
Nchimbi amesema wanasiasa akitoa mfano wa madiwani wamekuwa wakisema wananchi
ni masikini na wa chini kauli zilizokuwa zikiwakatisha tama ya kuchangia
maendeleo kwa kiwango kikubwa na kujiona hawana uwezo huo.
“Mnawaita
wananchi wa chini nani amewaweka ninyi juu? Inapofika wakati wa michango ya
maendeleo mnasema wananchi ni masikini hawawezi kuchangia, nawaambia mkitoka
hapa kwenye mafunzo mkatubu na muifute kauli ya kuwaita masikini, wananchi hawa ni msingi wa
maendeleo na wana mchango mkubwa kwa maendeleo ya halmashauri” amesisitiza.
Ameongeza
kuwa kumekuwa na kutokuaminiana kati ya madiwani na watendaji hali inayowafanya
kutupiana lawama pale jambo linapoharibika badala ya kutafuta suluhu kwa pamoja ili
wananchi wapate huduma na maendeleo kwa haraka.
Dkt.
Nchimbi amesema mafunzo hayo waliyopewa yaonyeshe tofauti kati ya zamani na
sasa huku akisisitiza kutumia fursa zilizopo vizuri na halmashauri kusimamia na kuhakikisha wananchi
wananufaika na fursa zilizopo katika halmashauri yao.
Madiwani
na watendaji kwa kauli moja wamekubali kuwa kabla ya mafunzo kumekuwa na
kutokuaminiana na kusababisha shughuli kutofanikiwa kwa kukosa ushirikiano wa
wananchi, wanasiasa na watendaji wenyewe ila baada ya mafunzo wanasiasa na
watendaji watafanya kazi kwa kushirikiana na kuwahusisha wananchi ili wao ndio
waibue miradi na kuimiliki.
Diwani
Viti Maalumu kutoka kata ya Kinyangiri Eunice Kalaila amesema mafunzo hayo
yatawafanya waweze kusimamia fedha zinazotolewa na serikali ili ziweze
kukamilisha miradi kwa gharama na ubora sahihi.
Kalaila
ameongeza kuwa kutokana na mafunzo hayo utoaji wa taarifa utakuwa yakinifu huku
miradi yote iliyosimama kwa kukosa ushirikiano wa wananchi itaendelea na kukamilika
huku wananchi wataelimishwa kutambua fursa zilizopo na kuibua miradi yao
watakayoikamilisha wenyewe na si kuitegea serikali.
Kwa upande
wake Diwani Viti Maalumu kutoka Kata ya Ibaga Habiba Issa amemkabidhi mkuu wa
mkoa matunda ya asili aina ya furu huku akisisitiza kuwa sasa vijana
wataelekezwa kutambua fursa zilizopo kuliko kusubiria ajira za serikali huku akitoa mfano wa
fursa ya kutengeneza juice kutokana na matunda hayo ya asili.
Naye
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mkalama Godfrey Sanga amesema atahakikisha
anasimamia maelekezo yote ili wananchi wake wapate huduma nzuri na maendeleo kwa
haraka huku akiamini lawama na malalamiko yatapungua.
Sanga
amesema sasa hakuta kuwa na uhasama kati ya watendaji na wanasiasa na hivyo
ushirikiano huo utasaidia katika kuibua na kusimamia miradi pamoja na kutambua
na kuzitumia fursa za maendeleo zilizopo Mkalama.
Madiwani na watendaji kutoka halmashauri ya Mkalama wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi alipokuwa akizungumza nao kabla hajawapatia madiwani vyeti vya mafunzo ya usimamizi wa miradi na jitihada za jamii za mbinu za kutambua fursa na vikwazo.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akipokea na kufurahia zawadi ya matunda asilia aina ya furu kutoka kwa Diwani Viti maalum kata ya Ibaga Habiba Issa mara baada ya mafunzo ya usimamizi wa miradi na jitihada za jamii za mbinu za kutambua fursa na vikwazo, matunda aina ya furu yanaweza kutengenezwa juice na kuwa fursa ya ajira kwa vijana.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Rehema Nchimbi akimuonyesha Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhandisi Jackson Masaka zawadi ya matunda asilia aina ya furu aliyopewa na Diwani Viti maalum kata ya Ibaga Habiba Issa, matunda hayo yanaweza kutengenezwa juice na kuwa fursa ya ajira kwa vijana.
No comments:
Post a Comment