Friday, October 28, 2016

MKUU WA MKOA AAGIZA KIJANA YATIMA MWENYE MATATIZO YA NJIA YA HAJA KUBWA APEWE MATIBABU BILA MALIPO.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Mhandisi Mathew John Mtigumwe  amefanya ziara katika hospitali ya Wilaya ya Manyoni kukagua huduma zinazotolewa katika kliniki tembezi ya madaktari bingwa  na kuagiza kijana yatima aliyeishi miaka 16 bila sehemu ya haja kubwa kupatiwa matibabu bila malipo.

Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe ametoa agizo hilo wakati akitembelea wodi ya wanaume ambapo amekutana na kijana yatima Mabu Jisinza mwenye umri wa miaka 16 mkazi wa kijiji cha Mgandu wilayani Manyoni ambaye mara baada ya kuzaliwa bila sehemu ya kutolea haja kubwa alifanyiwa upasuaji wa kuwekewa njia ya muda sehemu ya tumboni na baada ya wazazi wake wote kufariki amekosa msaada wa kuwekewa njia ya kudumu.

Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe amemuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari John Mwombeki kuhakikisha anasimamia kijana huyo anapatiwa matibabu stahiki kwakuwa ameishi kwa kunyanyapaliwa kwa muda wa miaka 16 kutokana na kutoa haja kubwa sehemu ya tumbo huku akisaidiwa na msamaria mwema Lilema Luhumbika mkazi wa kijiji cha Mgandu ambaye amekuwa akimpa chakula na malazi.

Aidha Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe amemuagiza pia  Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Manyoni kuchangia fedha endapo kijana huyo atapewa rufaa zaidi na atakapopona apelekwe shule kwakuwa hajui kusoma, kuandika wala lugha ya Kiswahili.

Wakati huo huo Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe ametoa maelekezo kwa Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Daktari Fransis Mwanisi kuwa ndani ya mwezi mmoja awe ameanzisha kliniki ya magonjwa yasioambukiza baada ya kupata maombi kutoka kwa mgonjwa wa Kisukari Neema Jakson Mbijima aliyeomba kupatiwa huduma ya ushauri kwa wagonjwa wa kisukari, presha na magonjwa ya moyo.

Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe ameagiza pia kuongezwa kwa siku za kutolewa huduma hizo za kibingwa zilizoanza kutolewa wilayani Manyoni siku  jumatatu ya  tarehe 24 Oktoba na kutarajiwa kukamilika tarehe 28 Oktoba 2016 siku ya ijumaa, akielekeza kuwa wagonjwa wote watakaoandikishwa mpaka siku ya ijumaa wahudumiwe wote.

Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari John Mwombeki amesema kliniki tembezi ya madaktari bingwa Wilayani Manyoni inao madaktari bingwa wa macho, meno, watoto, daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama, daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na daktari bingwa wa upasuaji huku kwa muda wa siku tatu madaktari hao wameona wagonjwa 1038.

Mheshimiwa Mhandisi Mtigumwe amezungumza na wagonjwa waliojitokeza kupata huduma hizo na kuwataka wawataarifu wananchi wengine wajitokeze kwa wingi wasikiapo matangazo ya huduma za kibingwa kwa kuwa huduma za kibingwa kwa ngazi za wilaya ni nadra kupatikana na zitawapunguzia gharama na muda wa kufanya kazi za kuzalisha mali, ameongeza kuwa Mkoa unaweka utaratibu wa kufanya huduma hizo kuwa endelevu.

Huduma za Kliniki tembezi za madaktari bingwa ukiwa ni utaratibu wa kipekee kufanyika Mkoani Singida umezinduliwa tarehe 14 Agosti 2016 Wilayani Iramba katika hospitali ya Kiomboi ambapo jumla ya wagonjwa 1452 walionwa na mwezi Septemba huduma hiyo imetolewa katika halmashauri ya Wilaya ya Singida ambapo wagonjwa 1064 walinufaikana na sasa ikiwa ni zamu ya halmashauri ya Manyoni ambapo tayari wagonjwa 1038 wamehudumiwa, utaratibu huu utaendelea mwezi Novemba kwa halmashauri ya Ikungi.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Mhandisi Mathew J. Mtigumwe (katikati) akizungumza na wagonjwa waliojitokeza kupata huduma za madaktari bingwa, kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida Daktari John Mwombeki na kulia kwake ni Mkurugenzi wa halmashauri ya Manyoni Charles Fussi.
  

Wananchi wa Wilaya ya Manyoni waliojitokeza kupata huduma ya Kliniki tembezi ya madaktari bingwa.


Akina mama wa Wilaya ya Manyoni wakizungumza na Mkuu wa  mkoa wa Singida Mhe. Mhandisi Mathew J. Mtigumwe wakisubiri kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.


No comments:

Post a Comment