Monday, October 31, 2016

MKUU WA WILAYA YA MANYONI AWAOMBA WADAU KUENDELEA KUCHANGIA BWENI LA WASICHANA LILOUNGUA




Waheshimiwa madiwani wa halmashauri za Itigi na Manyoni wakijiandaa na mechi ya kuchangia bweni la wasichana lililoungua la sekondari ya Mwanzi Wilayani Manyoni.
 
Veronika-Manyoni.Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mhe. Geoffrey Idelphonce Mwambe, amepokea mifuko 54 ya cement yenye thamani ya tshs 800000 kutoka kwa Wanafunzi waliowahi kusoma katika Shule ya Sekondari Mwanzi ili kukamilisha ujenzi wa bweni la Wasichana Mwanzi Sekondari iliyopo Wilaya ya Manyoni Mkoani wa Singida.
Akiwashukuru wadau hao Mhe. Mwambe amesema kuwa anawashukuru wadau hao kwani wanaisaidia serikali katika kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa bweni la Wasichana kwa wanafunzi wa Shule hiyo ya Sekondari.
Mhe. Mwambe amesema kuwa wamefarijika kuona mchango huo ambao umekuja wakati muafaka wa kuwasaidia wanafunzi ambao wamekuwa wakisoma na kulala kwenye mazingira magumu kutokana na kutokuwa na mahali pazuri na salama pa kulala hali ambayo inawafanya washindwe kusoma vizuri.
Aidha amewaomba wadau wengine nao kujitokeza ili kuhakikisha wanakamilisha zoezi hilo mapema iwezekanavyo na anaamini watafanikiwa kwani wadau mbalimbali wameonesha moyo wa kusaidia watoto wao waondokane na adha hiyo ambapo hadi sasa bado zinahitajika Milioni 20 ili kukamilisha ujenzi wa bweni hilo.
Kwa upande wake  Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi Mh Ally John Minja  na Mwl. Veronica Mpanda walioongoza ujumbe huo wakiwawakilisha wenzao waliowahi kusoma katika Shule hiyo wamesema kuwa lengo la kutoa msaada huo ni kuwawezesha Wanafunzi wa kike kupata bweni jipya haraka iwezekanavyo. 


Wakati huo huo Waheshimiwa Madiwani wa Wilaya ya Manyoni wamecheza mechi ya hisani ili kuchangia ujenzi wa bweni la wasichana la Mwanzi Sekondari iliyopo Wilayani Manyoni, Mkoani Singida.
Waheshimiwa madiwani hao walifikia uamuzi huo ili kuisaidia Serikali katika ujenzi wa bweni hilo la wasichana lililoungua moto mapema mwezi Septemba Mwaka huu. 
Mechi hiyo ya hisani ilichezwa jana tarehe 30 Oktoba, 2016 katika viwanja vya St. Gasper Itigi na kuzikutanisha timu za Waheshimiwa Madiwani wa Manyoni Mashariki na Manyoni Magharibi ambapo hadi kukamilika kwa mechi hiyo matokeo yalikua ni goli 1-1.
 Jumla ya Shilingi 700,000 zilifanikiwa kukusanywa katika mechi hiyo ikiwa ni michango ya wadau mbalimbali walioshiriki katika uhamasishaji kupitia mchezo huo. 
Bweni la wasichana wa Shule ya Sekondari Mwanzi Wilayani Manyoni
lenye uwezo wa kubeba wanafunzi 48 liliteketea kwa moto usiku wa tarehe 9 Septemba, 2016 na kuwaacha wanafunzi hao wakiwa hawana mahali pa kulala.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Manyoni Mhe. Leonard Matonya na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Itigi Mhe. Ally Minja,  Halmashauri zinazounda Wilaya ya Manyoni  wamewashukuru Waheshimiwa Madiwani kwa kujitoa kwao kulikofanikisha kupatikana kwa kiasi hicho cha fedha lakini pia wakaomba wadau mbalimbali wa maendeleo kuendelea kujitolea misaada ya hali na mali ili kufanikisha ujenzi wa Bweni hilo la wasichana kwani bado kinahitajika kiasi cha Shilingi milioni 20 kukamilisha ujenzi wa Bweni la Wasichana Mwanzi Sekondari.
Waheshimiwa madiwani wa halmashauri za Itigi na Manyoni wakijiandaa na mechi ya kuchangia bweni la wasichana lililoungua la sekondari ya Mwanzi Wilayani Manyoni.

No comments:

Post a Comment