Monday, October 10, 2016

WAHADZABE WA KIJIJI CHA KIPAMBA SINGIDA WAANDIKISHWA KUPATA MGAO WA TASAF

Wahadzabe wa kijiji cha Munguli, kitongoji cha Kipamba Wilayani Mkalama Mkoa wa Singida wakiwa katika makazi yao.

Jumla ya Wahadzabe 136 kati ya 138 wakazi wa kijiji cha Kipamba wilaya ya Mkalama mkoani Singida wameandikishwa kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini TASAF III na wamenza kufaidika kuanzia Septemba mwaka huu hadi sasa.

Kundi la kabila la Wahadzabe ambalo linadaiwa kuwa limesahaulika bado linaishi maisha ya kijima na linategemea asali, matunda pori, mizizi ya miti na nyamapori kama chakula chao kikuu.

Imedaiwa kuwa kutokana na changamoto za tabia nchi na makundi ya wafugaji kuvamia pori la kijiji cha Kipamba vyakula hivyo vya asili havipatikani kwa kiwango cha kukidhi mahitaji.

Hayo yamesemwa mwishoni mwa wiki na mratibu wa TASAF mkoa wa Singida Patrick Kasango wakati akitoa taarifa yake ya utekelezaji wa mpango wa TASAF III mbele ya wawakilishi kutoka benki ya dunia, shirika la kazi dunia (ILO) na UNDP ambao wamefanya ziara ya kikazi mkoani hapa kukagua utekelezaji wa mpango huo.

“Lengo kuu la kuandikisha kundi la Wahadzabe katika mpango huu wa TASAF III ni kulisaidia kundi hilo kuanzisha miradi ya ufugaji kuku na mbuzi,ili kujipatia kipato Pia kuongeza mahudhurio shuleni kwa watoto wa kundi hilo, pamoja na vituo vya kutolea huduma za afya.Vile vile kuongeza mahudhurio ya akina mama kuhudhuria kliniki”, alifafanua Kasango.

Katika hatua nyingine Mratibu huyo alisema kuwa TASAF III mkoani hapa imetumia zaidi ya shilingi 18.8 bilioni kwa ajili ya kunusuru kaya masikini 40,218, kati ya septemba mwaka huu hadi sasa.

Hata hivyo alisema kuwa kaya 281 zimeondolewa katika mpango huo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya vifo vya walengwa.

Kati ya fedha hizo shilingi 430,357,208.08 zimetumika kugharamia ujenzi wa zahanati nne na nyumba mbili za kuishi watumishi wa afya na elimu.

Aidha alisema fedha zingine shilingi 562,755,000 zimetumika kununulia vifaa vinavyotumika kwenye miradi ya ujenzi inayotoa fursa za ajira za muda kwa walengwa.

“Ajira hizi za muda zimelenga kuziongezea kipato kaya zilizoandikishwa kwenye mpango wa TASAF 111 na wakati huo huo,kaya hizo zitakuwa zimeshiriki kuondoa kero zinazowakabili katika maeneo yao,ikiwemo uhaba mkubwa wa maji”,alisema.

Mratibu Kasango alisema pamoja na mafanikio hayo ya kujivunia bado wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya uhaba wa magari, barabara mbovu ambazo wakati wa masika hazipitiki na baadhi ya kaya kutembea mwendo mrefu kufika kwenye kituo cha kuhaulisha fedha na baadhi ya maeneo kutokuwa na huduma za simu.
 
Mwenyekiti wa kijiji cha Kipamba Edward Mashimba Mkumbo pamoja na kuipongeza serikali na wadau wengine kwa kulishirikisha kundi la Wahadzabe kwenye mpango wa huo ameiomba serikali kuwajengea barabara ya kupitika wakati wote.

“Kama mpango huu usingeanzishwa huku kwetu hali ingekuwa mbaya sana kwa sababu vyakula vyetu vya asili havipatikani tena na sisi kama mnavyojua hatuna utamaduni wa kulima. Niiombe tena serikali itupatie wahudumu wa afya kwani toka jengo la zahanati hiyo likamilike miaka kadhaa iliyopita hatujapatiwa mhudumu, Pia tupatiwe hati miliki ya eneo letu,” alisema.

Kwa upande wake mkurugenzi uratibu TASAF makao makuu, Alphonce Kyariga ameishauri TASAF mkoani hapa, kuhakikisha taarifa zao zinakuwa na takwimu, kwa madai kwamba zikiwa na takwimu zitakuwa chachu kwa serikali na wadau wengine kuzipatia ufumbuzi wa kudumu changamoto husika.

Naye mwakilishi wa benki ya dunia Wolter Soer alisema kwa kiwango kikubwa timu yao imeridhishwa na utekelezaji wa TASAF mkoani Singida na kuahidi kwamba wataendelea kushirikiana na serikali ya awamu ya tano kuendeleza mpango huo.

“Kwa upande wa kundi la Wahadzabe tumeguswa zaidi na kwamba tutachukua hatua maalum katika kulisaidia kundi hili.Tunataka ifike wakati na Wahadzabe wawe na maisha bora kama walivyo Watanzania wengine,” alisema Soer.
Mwakilishi wa  Benki ya dunia Wolter Soer akitoka nje mara baada ya kutembelea moja ya nyumba ya wahadzabe wa kitongoji cha Kipamba wilayani Mkalama Mkoani Singida.

Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida Patrick Kassango akizungumza na wawakilishi wa benki ya dunia, shirika la UNDP na shirika la kazi dunia walipotembelea kitongoji cha kipamba Wilayani Mkalama mkoani Singida.

No comments:

Post a Comment