Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J Mtigumwe (katikati)
akizungumza na wagonjwa, kulia kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John
Mwombeki na kushoto ni Mkurugenzi wa tiba kutoka wizara ya afya Dokta
Magreth Mhando.
Wizara ya afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Watoto na
Wazee imeishauri mikoa yote ya Tanzania bara kuiga mfano wa mkoa wa Singida wa
kuanzisha huduma za kibingwa za mkoba kwa ngazi za wilaya ili kuwafikia
watanzania wengi wenye uhitaji.
Mkurugenzi wa tiba
kutoka wizara hiyo Dokta Magreth Mhando ametoa ushauri huo katika hospitali ya
Mtakatifu Calorus Mtinko Singida Vijijini alipotembelea kujionea awamu ya pili
ya zoezi la huduma za kibingwa za Mkoba.
Dokta Mhando amesema
kumekuwa na huduma za kibingwa za mkoba ila hazikufanyika vizuri kama ambavyo mkoa wa Singida umekuwa
ukifanya na kutoa pongezi za Wizara kwa Mkuu wa mkoa na Mganga mkuu wa mkoa kwa
ubunifu huo.
Amesema huduma za
kibingwa za mkoba zimekuwa zikiratibiwa na taasisi au hospital kubwa kama
Muhimbili ambapo madaktari bingwa wamekuwa wakitoa huduma kwa ugonjwa fulani na
kwa ngazi ya hospitali za Mkoa tofauti na zoezi linaloendelea Mkoani Singida la
kutoa huduma za kibingwa kwa magonjwa mbalimbali.
Dokta Mhando
ameongeza kuwa kutokana na uhaba wa madaktari bingwa nchini wizara imetenga fedha
kwa ajili ya kuwasomesha madaktari na kuwashauri waajiri ambao ni makatibu
tawala wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya
kuwasomesha madaktari hao kwakwuwa wizara pekee haitaweza.
Amesema utaratibu ni
kuwa na madaktri bingwa angalau watano kila Mkoa lakini mikoa mingi haina idadi
hiyo huku akiongeza kuwa lengo la kutembelea zoezi hilo Singida nikujionea hali
halisi na sio kusubiria taarifa.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhandisi Mathew John Mtigumwe mara baada ya kutembelea wodi zote na
kuzungumza na wagonjwa waliopata huduma za kibingwa amemtaka Mganga Mkuu wa
Mkoa kuongeza muda wa kutoa huduma hiyo kutoka siku tano hadi nane kutokana na
wingi wa wagonjwa waliojitokeza.
Mhandisi Mtigumwe
amesema huduma hiyo inasaidia kutambua magonjwa na kuyatibu kabla hayajawa sugu
lakini pia gharama zikiwa nafuu kutokana na kusogezwa kwa ngazi za halmashauri.
Ameongeza kuwa lengo
la ofisi yake ni kuhakikisha huduma za kibingwa za mkoba zinapelekwa kwa kila
halmashauri na endapo zoezi likikamilika na kukiwa na uhitaji mkubwa kuna
uwezekano mkubwa wa kurudia zoezi hilo.
Mhandisi Mtigumwe
amesema kuelekea Tanzania ya viwanda afya bora ni muhimu na wazalishaji wakubwa
ni wananchi wa ngazi za chini hivyo huduma hiyo itasaidia kuimarisha afya ili
waweze kuzalisha bidhaa kwa wingi na
zenye ubora.
Amesema kwa wale
wagonjwa watakaopewa rufaa kwenda nje ya Mkoa utaratibu utaangalia wa kuwapatia
usafiri wa Mkoa ili kuwapeleka hasa wale wasiojiweza.
Naye Mganga Mkuu wa
Mkoa Dokta John Mwombeki amesema kwa muda wa siku tano wagonjwa zaidi ya 800
wameonana na madaktari bingwa huku idadi ikitarajiwa kuongezeka kutokana
nakuongezwa kwa siku za klutoa huduma.
Dokta Mwombeki
amesema wagonjwa wengi wanaofika wanatoka maeneo mbalimbali hasa maeneo ya
kijijini na wenye hali duni ya maisha hivyo zoezi hilo limesaidia wananchi hasa
wwenye kipato cha chini.
Amesema madaktari
bingwa wanaotoa huduma za kibingwa za mkoba ni madaktari bingwa wa magonjwa ya
akina mama, watoto, macho, meno, magonjwa ya ndani na daktari bingwa wa
upasuaji.
Wagonjwa waliopata
huduma wameushukuru uongozi wa mkoa kwa kubuni utaratibu wa kuwafuata wagonjwa
karibu ili kuwapatia huduma za kibingwa kwakuwa inawasaidia kupata matibabu
mapema kabla magonjwa hayajawa sugu na kushauri huduma iwe endelevu angalau
kila mwaka.
Wagonjwa waliofanyiwa operesheni ya macho na madaktari bingwa wakizungumza na Mkuu wa Mkoa (hayupo).
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J Mtigumwe (katikati)
akizungumza na mgonjwa (hayupo pichani), kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John
Mwombeki.
Wagonjwa wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa alipowatembelea na kuona huduma za mkoba za kibingwa zikiendelea kutolewa, wagonjwa hao walikuwa wakisubiri kuonana na daktari bingwa wa magonjwa ya akina mama.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J Mtigumwe akisikiliza maoni ya wagonjwa waliokuwa wakisubiri kupata huduma za kibingwa kushoto kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John
Mwombeki na anayefuata wa kwanza ni Mkurugenzi wa tiba kutoka wizara ya afya Dokta
Magreth Mhando.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J Mtigumwe
akitembelea na kukagua huduma wanazopatiwa wagonjwa wa huduma za kibingwa katika hospitali ya Mt calorus Mtinko, kulia kwake ni Mganga Mkuu wa Mkoa Dokta John
Mwombeki na kushoto ni Mkurugenzi wa tiba kutoka wizara ya afya Dokta
Magreth Mhando.
No comments:
Post a Comment