Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Mkuu
wa Wilaya ya Manyoni Mh. Geoffrey Idelphonce Mwambe amewasimamisha kazi
watumishi watano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kwa kushindwa kutekeleza
majukumu yao vizuri, uzembe na utovu wa nidhamu.
Mwambe
amefanya uamuzi huo alipokuwa kwenye Mkutano na Wafanyakazi wa Halmashauri ya
Wilaya ya Manyoni leo Tarehe 29.09.2016, ambapo aliwataja Watumishi hao
aliowasimamisha kazi kuwa ni Mkuu wa Idara ya Ugavi Bw. Genesius Rugemalira
ambaye amesimamishwa kwa kushindwa kusimamia manunuzi ya Halmashauri na
kuisababishia Serikali hasara ya Tshs. Mil 16, Daktari John Amita wa Hospitali
ya Wilaya ya Manyoni aliyesimamishwa kazi kwa tuhuma za kupigana na daktari
mwenzake hospitalini hapo, tuhuma za utoaji mimba, na uzembe uliopelekea kifo
cha mama mjamzito.
Wengine
waliosimamishwa ni Muuguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni Bw. Mika Iloti kwa
uzembe uliopelekea kifo cha Mama mjamzimzito, Msaidizi wa Ofisi Bw. Anthony
Sanga kwa ufujaji wa mapato ya Halmashauri na Mtendaji wa Kijiji cha Makasuku Bw.
Mussa Ndahani ambaye kwa kushirikiana na Mwenyekiti wa Kijiji chake wamekuwa
wakitoa vibali vya uvunaji Misitu kwa Wafanyabiashara ya mbao bila kuzingatia sheria
na taratibu kwa kofia ya zoezi la utengenezaji wa madawati linaloendelea.
Mh.
Mwambe amemwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kuhakikisha
Watumishi hao wanasimamishwa mara moja kupisha uchunguzi wa tuhuma
zinazowakabili ili hatua Zaidi za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
Wakati
huo huo Mkuu huyo wa Wilaya ya Manyoni ametoa karipio kali na kumwagiza
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Bw. Charles Edward
Fussi kuwachukulia hatua Mganga Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Dkt. Francis Mwanisi
kwa kuficha taarifa na kufumbia macho matukio ya utovu wa nidhamu wa Madaktari
na wauguzi wa Hospitali ya Wilaya ya Manyoni na Mhasibu Mkuu wa mapato Bw.
Elias Mwachinyemba kwa kushirikiana na wazabuni wa ukusanyaji mapato ya Halmashauri
waliomaliza muda wao kuhujumu mapato ya Halmashauri.
Mh.Mwambe
pia ametengua uteuzi wa Kaimu Mkurugenzi wa Mji mdogo wa Manyoni, Bw. Yona
Chalinze na Kaimu Mhandisi wa Maji Bw. Musoma Kanyere kwa utendaji kazi
usioridhisha.
Akitoa
maamuzi hayo Mh. Mwambe amewaeleza Watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya
Manyoni kuwa ni lazima waelewe kuwa wao sio tu Watumishi wa Serikali bali ni
Watumishi wa Umma hivyo wana wajibu kuutumikia umma kwa weledi, kujituma,
uadilifu na kuacha kufanya kazi kwa mazoea lakini pia kuepuka vitendo vya
Rushwa.
Imetolewa
na:
Veronica
D. Luhaga,
Afisa
Habari,
HALAMASHAURI
YA WILAYA
MANYONI.
0786-848497
No comments:
Post a Comment