Thursday, September 15, 2016

RAIS MAGUFULI ATOA ZAWADI KWA KAMBI YA SUKAMAHELA, SINGIDA.



Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt.Angelina Lutambi (wa tatu kulia) akimkabidhi Clodia Madori baadhi ya zawadi zilizotolewa na Rais Magufuli kwa ajili ya wazee na walemavu wasiojiweza wa Makazi ya Sukamahela ili waweze kuungana na Watanzania wengine kusherehekea siku kuu ya Idd Elhaj.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. John P. Magufuli ametoa zawadi ya sikuu ya Eid al Hajj kwa wahudumiwa 65 wa makazi ya wazee na walemavu wasiojiweza ya Sukamahela Wilayani Manyon.

Mhe Rais ametoa zawadi ya mchele kilo 120, mafuta ya mboga lita 20, mbuzi watatu, kilo 10 za sukari, kilo 10 maharage, mafuta ya kupikia lita 10, nyanya na vitunguu kwa wakazi hao kama ilivyo desturi yake katika sikukuu zote katika kuonyesha kuwajali na kuwathamini.

Akikabidhi zawadi hizo kwa niaba ya Mhe Rais, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi amesema zawadi hizo zimetolewa na Mhe Rais ili wahudumiwa wa makazi ya Sukamahela washerehekee sikukuu kama wananchi wengine.

Dkt. Lutambi alitembelea jiko ambalo hupikiwa chakula cha wahudumiwa hao ambapo alibaini changamoto ya wapishi ambao hulewa wakati wa kazi licha ya kuwa wachache, pia alibaini uhaba wa chakula ambapo wahudumiwa hutegemea mlo mmoja wa msaada kutoka kwa shirika la masista wa Damu azizi ya yesu.

Dkt. Lutambi alitoa onyo kali na kumwagiza Mkuruguzeni wa Halmashauri kuwapa mwezi mmoja wa kujirekebisha wapishi hao pamoja na afisa ustawi wa jamii wa kituo hicho wasipojirekebisha wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Aidha wahudumiwa hao walitoa changamoto mbalimbali ikiwemo ukosefu wa kuni, chakula cha zawadi ya rais kutumika vibaya na viongozi wa makazi hayo wasiokuwa waadilifu na hivyo alimwagiza mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya Manyoni kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu kero zinazowakabili wakazi wa kambi hiyo.

Aliongeza kuwa katika makazi hayo kuna watoto waliotelekezwa na wazazi wao kwa kuwaachia wazee wa kambi hiyo ambao hawana uwezo na kuagiza wazazi wao wasakwe na kukabidhiwa watoto wao.

“Kuna hatari kubwa watoto hawa wakakosa haki yao ya msingi ya kupata elimu. Wazazi hawa watafutwe kwa nguvu zote, ili wakabidhiwe watoto wao waweze kuwapatia mahitaji muhimu kwa maisha yao,” alisema Dk.Lutambi.

Kwa upande wao wahudumiwa wa makazi hayo wameeleza changamoto ya uwepo wadudu kama kunguni, papasi na panya wanaowasumbua hasa wazee.

Wamedai kunguni hao wamekuwa kero kwa muda mrefu ambayo haijapatiwa ufumbuzi hadi sasa, licha ya kutoa malalamiko hayo mara nyingi.

Akizungumza kwa niaba ya wakazi hao, Cleodia Madori (68), alisema wakazi wengi wa kambi hiyo ni wazee ambao kwa kawaida damu zao ni chache.

“Mtu mzee mwenye damu chache ambazo zikinyonywa na kunguni,mhusika anaathirika zaidi kiafya.Tumepeleka mara nyingi vilio vyetu kwenye ngazi mbalimbali za uongozi juu ya kunguni ambao wanasababisha tusilala usiku kucha.Lakini hadi sasa hakuna hatua zo zote zilizochukuliwa,” alisema Madori kwa masikitiko.

Kwa upande wake Daniel Kipande, alisema kambi yao ina changamoto ya uhaba wa madawa ya kutibu vidonda vya ukoma, na nyumba zao ni chakavu hazijafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu.

Aidha, alisema zawadi mbalimbali ikiwemo mchele ambazo zimekuwa zikitolewa na ofisi ya rais kwa ajili ya wakazi hao wakati wa sikukuu mbalimbali, baadhi ya watumishi wa kambi hiyo wamekuwa wakijinufaisha binafsi.

“Kwa mfano leo tumepatiwa na rais wetu Magufuli mchele kilo 120, siku ya siku kuu ya Idd Alhaj,tutapikiwa kilo 30 tu, baada ya hapo hatutaona tena mchele huu. Tunaomba mkuu wa wilaya ya uliangalie hili,” alisema Kipande na kushangiliwa kwa nguvu na wenzake.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya Manyoni, Charles Susi, aliahidi kumtuma Afisa afya Septemba 13, mwaka huu, kufanya tathimini kiasi cha dawa ya kuangamiza kunguni na wadudu wengine katika kambi hiyo.

“Pia tunakwenda kuangalia uwezekano wa kuleta mitungi mikubwa ya gesi kwa ajili ya matumizi ya kupikia chakula. Ndugu zetu hawa wametoa lalamiko la uhaba wa kuni,kuni za kupikia chakula katika maeneo haya hakuna hivyo mbadala wa kuni ni gesi tu,” alisema.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe amesema atahakikisha anaitembelea kambi hiyo mara kwa mara kuangalia namna Mkurugenzi anavyo shughulikia changamoto hizo.

Mwambe amesema walezi wa watoto waliofikia umri wa kusoma ambao wapo katika kambi hiyo wote wapelekwe shule na atakayekaidi hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina Lutambi akizungumza kwenye hafla ya makabidhiano ya zawadi mbalimbali ikiwemo mbuzi wawili zilizotoilewa na Rais Dkt. Magufuli kwa ajili ya wazee na walemavu wasiojiweza wa makazi ya Sukamahela wilaya ya Manyoni, wa kwanza kulia ni mbunge wa jimbo la Manyoni Mashariki Daniel Mtuka na anayefuatilia ni Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Geofrey Mwambe.


Mkazi wa makazi ya wazee na walemavu wasiojiweza wa makazi ya Sukamahela Wilayani Manyoni Clodia Madori akitoa shukrani kwa Rais Dk.Magufuli kuwakumbuka kwa zawadi ili waweze kuungana na Watanzania wengine kusherehekea siku kuu ya Idd Elhaj.


Picha na Nathaniel Limu.

No comments:

Post a Comment