Friday, September 16, 2016

MKUU WA MKOA WA SINGIDA AWAASA WAJUMBE WA ALAT KUTATUA KERO ZA HALMASHAURI.




Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe akiwaasa wakurugenzi, meya na wenyeviti wa halmashauri zote saba Mkoani Singida  katika kikao cha Jumuiya za Serikali za mitaa Tanzania (ALAT).

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amewaasa wakurugenzi, meya na wenyeviti wa halmashauri zote saba Mkoani Singida kutumia vikao vya mafuzo ya Jumuiya za Serikali za mitaa (ALAT)  kutatua kero za halmashauri.

Mhandisi Mtigumwe ameyasema hayo wakati akifunga mafunzo ya ALAT mkoa wa Singida na kuwasisitizia kuwa mafunzo hayo yawe na tija na sio kukaa vikao visivyo na matokeo chanya.

Ameongeza kuwa katika kipindi cha miezi sita tangu ateuliwe na Mhe Rais amebaini halmashauri zina changamoto za ukusanyaji hafifu na usioridhisha wa mapato ya ndani pamoja na mikataba mibovu inayosainiwa na halmashauri na hivyo kuiletea hasara serikali.

Mhandisi Mtigumwe amesema kumekuwa na migogoro ya ardhi inayosababishwa na maafisa ardhi wasio kuwa waadilifu, watumishi na madiwani kujimilikisha ardhi na vibanda kinyume na utaratibu pamoja na kutotengwa kwa asilimia kumi ya mapato ya ndani kwa ajili ya wanawake na vijana.

“Halmashauri hazijatenga maeneo ya viwanda vidogo na vya kati, uchafu umekithiri katika maeneo mengi, watumishi wanaokiuka taratibu hawachukuliwi hatua za kinidhamu na mawasiliano hafifu kati ya viongozi na watumishi, viongozi na viongozi na hata watumishi wenyewe, hizi ni baadhi ya changamoto ambazo kikao cha ALAT kitumike kuzitafutia majibu, alisisitiza.

Mhandisi Mtigumwe amewasisitiza wakurugenzi kuunda mabaraza ya wafanyakazi na halmashauri zenye mabaraza hayo basi vikao vifanyike ili kero na changamoto za watumishi zisikilizwe na kutafutiwa ufumbuzi.

Kwa upande wao meya, wenyeviti na wakurugenzi wa halmashauri wamemshukuru mkuu wa Mkoa kwa nasaha alizowapa na kuahidi kuyatumia mafunzo ya ALAT katika kuleta mabadiliko katika halmashauri zao.

Wajumbe walipata fursa ya kujifunza juu ya Mfumo ya serikali za mitaa Tanzania bara, ukusanyaji wa mapato ya ndani kwenye halmashauri, utaratibu wa manunuzi katika serikali za mitaa, uwazi na uwajibikaji na mawasiliano kwa viongozi.
Wakurugenzi, meya na wenyeviti wa halmashauri zote saba Mkoani Singida wakiendela na katika kikao cha Jumuiya za Serikali za mitaa Tanzania (ALAT).

Wakurugenzi, meya na wenyeviti wa halmashauri zote saba Mkoani Singida  wakiendela na katika kikao cha Jumuiya za Serikali za mitaa Tanzania (ALAT).

No comments:

Post a Comment