Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M. Lutambi akiupokea mwenge wa uhuru kutoka Katibu Tawala Mkoa Dodoma Rehema S. Madenge.
Mkoa wa Singida umepokea mwenge wa uhuru mapema asubuhi kutoka mkoani Dodoma ili uweze kukimbizwa katika halmashauri zote saba, uzindue, utembelee na utaweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akiupokea mwenge huo kutoka kwa Katibu Tawala
Mkoa wa Dodoma Bi. Rehema S. Madenge katika Kijiji cha Lusilile Kata ya
Kintinku Wilaya ya Manyoni, Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Angelina M.
Lutambi amesema jumla ya miradi 61 yenye thamani ya shilingi bilioni 14
itazinduliwa, itatembelewa na kuwekewa mawe ya msingi.
Dkt. Lutambi ameongeza kuwa miradi hiyo
imejikita katika sekta za ufugaji, mazingira, maji, afya, elimu, barabara,
utawala bora, kilimo, kshirika, biashara, ardhi pamoja na programu za mapambano
dhidi ya dawa za kulevya, malaria, rushwa na ukimwi.
Amesema wananchi na viongozi kwa pamoja wako
tayari kuukimbiza mwenge wa uhuru mkoani Singida, kuulinda kuuenzi na kudumisha
upendo amani na mshikamano wa Taifa letu ulioasisiwa na baba wa Taifa Hayati
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa mara ya awali juu ya kilele cha Mlima
Kilimanjaro Disemba 9, 1961.
Mara baada ya kuupokea mwenge huo, Katibu
Tawala Mkoa wa Singida Dokta Lutambia alimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Manyoni
Geofrey Mwambe ili aanze kuumbiza katika halmashauri yake, utembelee, uzindue
na kuweka mawe ya msingi katika miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Manyoni
Geofrey Mwambe amesema Mwenge huo unatarajiwa kuzindua miradi saba yenye thamani ya shilingi milioni
831,719,569.
Mwambe ameongeza kuwa miradi itakayozinduliwa
ni pamoja na uzinduzi wa programu ya ufuatiliaji na kuteketeza mbu, kufungua mradi
wa ujenzi wa vyumba viwili vya madarasa na matundu nane ya vyoo na ukarabati wa
vyumba viwili vya madarasa.
Miradi mingine ni ufunguzi wa daraja la
Makutupora, kuzindua klabu ya wapinga rushwa, kuzindua mradi wa ujenzi wa kituo
cha maarifa ya kupambana na UKIMWI, kuzindua mradi wa vijana wa kufyatua
matofali, na kuzindua klabu ya kupambana na dawa za kulevya.
Mbio za Mwenge wa uhuru kwa Mwaka 2016 zimebeba
kauli mbiu ya "Vijana ni nguvu kazi ya Taifa, Washirikishwe na
kuwezeshwa" ambapo hata hivyo kila Halamashauri nchini zimeelekezwa
kutenga asilimia 5% ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya vijana na asilimia 5%
nyingine kwa ajili ya kina mama.
Katika kumaliza mizizi wa rushwa, dawa za
kulevya, ukimwi na malaria Mwenge wa uhuru umejikita zaidi katika kauli mbiu ya
"Timiza wajibu wako kata Mnyororo wa Rushwa" kwenye mapambano dhidi
ya Rushwa, Kauli mbiu ni "Tujenge jamii, Maisha na Utu wetu bila dawa za
kulevya".
Kwenye Mapambano dhidi ya dawa za kulevya, kauli
mbiu ya "Tanzania bila maambukizi mapya, Unyanyapaa na Vifo vitokanavyo na
UKIMWI inawezekana" wakati kwenye
Mapambano dhidi ya Malaria kauli mbiu ni " Wekeza katika maisha ya baadae,
Tokomeza Malaria".
Kwa mujibu wa ratiba za mbio za Mwenge wa Uhuru
za mwaka huu, unakimbizwa katika Halmashauri na Manispaa zipatazo 183 na kilele
cha mbio hizo ni Octoba 14, katika Mkoa wa Simiyu.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M. Lutambi akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Mwenge wa uhuru ili uweze kukimbizwa katika halmashauri hiyo.
Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina M. Lutambi akiupokea mwenge wa uhuru kutoka mkimbiza mwenge kitaifa.
Kiongozi wa mbio za mwenge wa uhuru mwaka 2016 George Jackson Mbijima akisalimiana na Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Miraji Mtaturu mara baada ya kuwasili Mkoani Singida.
No comments:
Post a Comment