Friday, September 09, 2016

WAENDELEE WAIRWANA WAMKABIDHI MKUU WA MKOA WA SINGIDA MADAWATI ELFU MOJA.



Wanafunzi wa Shule ya Msingi Ilongero Wilayani Singida wakiwa wameketi katika madawati yaliyotolewa na asasi ya WAENDELEE.

Asasi isiyo ya Kiserikali ya wakazi wa tarafa za Ilongero, Mtinko na Mgori ya WAENDELEE yenye mkusanyiko wa watu wenye jamii ya Wairwana wamemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J Mtigumwe mchango wa madawati 1055 yenye thamani ya shilingi milioni 97,125,000.

Akiongea kabla ya kukabidhi mchango huo wa madawati Mwenyekiti wa WAENDELEE Joseph Jingu Kijeruda amesema asasi hiyo imeona umuhimu wa kutoa mchango huo ili kuunga mkono nitihata bza serikali katika kuhakikisha hakuna mwanafunzi anayekaa chini.
 
Kijeruda amesema asasi hiyo yenye lengo la Kuhamasisha na kushiriki katika maendeleo ya Wilaya ya Singida, imeguswa na changamoto za sekta ya Elimu zinazosababisha ufaulu duni kwakuwa wanafunzi wengi wa tarafa hizo tatu wamekuwa wakikaa chini wakati wa masomo.

Ameongeza kuwa makubaliano na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida ni kuyagawa madawati katika shule zenye upunguzu zaidi kuliko nyingine huku akiomba madawati hayo yawekwe kwenye kumbukumbu ya mali za serikali na kutunzwa vizuri.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew J. Mtigumwe ameishukuru na kuipongeza Asasi ya WAENDELEE kwa kuunga mkono agizo la Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania la kuhakikisha kila mwanafunzi ana kaa kwenye dawati ifikapo June 2016.

Mtigumwe amesema hadi kufikia Juni mwaka 2016 halmashauri za Iramba, Mkalama, Itigi, Ikungi na Halmashauri ya Manispaa zilikuwa zimekamilisha utengenezaji wa madawati huku Manyoni ikiwa bado haijakamilisha madawati 1,229 na halmashauri ya Wilaya ya Singida ikiwa haijakamilisha madawati 667.

Amewasisitiza na kuwaagiza wakuu wa Wilaya na wakurugenzi kufanya uhakiki wa madawati, viti na meza kwa shule za msingi na sekondari, kufanya tathmini ya mahitaji ya matundu ya vyoo kwa shule za msingi na sekondari, kufanya uhakiki wa mali zote za shule na kuhakikisha kuwa maeneo yote ya shule yanapimwa na kupatiwa hati.
 
Mwanzoni mwa mwaka 2016 mahitaji ya madawati kwa halmashauri ya wilaya ya Singida yalikuwa 16,556 huku upungufu ukiwa 6,122.
Hadi sasa kupitia jitihada mbalimbali kama vile harambee mbalimbali, mchango ya mfuko wa jimbo, mchango wa chama cha mapinduzi wilaya ya Singida, nguvu za wanakijiji na asasi ya WAENDELEE, halmashauri imefanikiwa kuvuka lengo na kupata madawati17,384 ikiwa na ziada ya madawati 828.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Eliya Digha akimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew J. Mtigumwe (aliyevaa miwani) mara baada ya kuyapokea madawati hayo yaliyotolewa na asasi ya WAENDELEE, katikati yao ni Mwenyekiti wa asasi hiyo Bw. Joseph J. Kijeruda.
Baadhi ya ndogo kati ya madawati 1055 yaliyotolewa na asasi ya WAENDELEE.

No comments:

Post a Comment