Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew J. Mtigumwe akimkabidhi Mkurugenzi wa Halmashauri ya Ikungi Rustika Turuka madawati yaliyochangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amekabidhi madawati 630 kwa wakurugenzi wa
halmashauri saba za Mkoa wa Singida yakiwa ni mchango wa wadau na taasisi
mbalimbali zilizojitolea kuunga mkono uchangiaji wa madawati mkoani hapa.
Katika makabidhiano
hayo yaliyofanyika katika Ukumbi wa
Ofisi za Mkoa Mtigumwe amesema kuwa hali ya Madawati ilikuwa chini ya
asilimia 40 lakini chini ya uongozi wake kwa kushirikiana na wadau 67 wa
Maendeleo wameweza kuchangia jumla ya shilingi milioni 42,626,500 na
kufanikisha lengo la utengenezaji wa madawati kwa asilimia 98.
Ameongeza kuwa upungufu
Mkubwa ulikuwa zaidi katika Halmashauri za Singida na Manyoni huku akiwataka Wakurugenzi
hao kuyachukua madawati hayo haraka na kuyapeleka Katika shule zenye upungufu
mkubwa ili kuboresha mazingira ya kujisomea.
Mtigumwe
ameeleza kuwa mwanzoni mwa mwezi June mwaka huu aliteua kamati ndogo ya uratibu
wa madawati kwa kushirikisha wadau mbalimbali katika Mkoa baada ya kuona juhudi
za serikali kupitia mamlaka za Halmashauri ya Manispaa na Wilaya na kamati hiyo
ilifanikiwa kukusanya milioni 42,626, 500.
Amesema
wadau waliojitokeza na kuunga mkono juhudi za halmashauri ni wadau 60 waliochanga
pesa taslimu 29,046,500, wadau watano waliotoa madawati 60 yenye thamani ya
shilingi 3,580,000 na kampuni ya Bonite Bottlers iliyotoa madawati 100 yenye
thamani ya shilingi 10,000,000.
Naye
Mwenyekiti wa kamati ya kuratibu harambee
ya madawati Elias Donaty Seng’ongo amefafanua kuwa kamati ilishirikisha wadau
mbalimbali na walioweza kushiriki ni pamoja na taasisi za serikali (TBA, Gispa,
Tanroads, Sido, Veta, Temesa, Sekretarieti ya Mkoa, Takukuru na TRA), Mashirika
ya huduma (NHC, Tanesco, Suwasa na Posta), taasisi za fedha (NMB na CRDB),
Mifuko ya hifadhi ya jamii (NHIF, NSSF, na PSPF) na Mashirika yasiyo ya
serikali (NGO’s, SEMA, HAPA, TUNAJALI, na HELVETAS).
Seng’ongo
amewataja wadau wengine waliochangia kuwa ni Vyuo na idara za serikali (NAO,
Madini, Hazina Ndogo, Chuo cha Uhasibu, TIA, Utumishi wa Umma, Chuo cha walimu
Singida, Abet English Medium School, Maasai English medium School, Lake School), Viwanda vya usagishaji
mafuta (Mount Meru na Umoja wa wakamuaji mafuta Mkoa wa Singida),
Wafanyabiashara mbalimbali, wauzaji wa vinywaji baridi (Bonite Bottles Ltd),
Wauzaji wa vipuri vya magari, Makandarasi, Wakala wa huduma za misitu TFSA, maduka
ya vifaa vya ujenzi, Hoteli, Baba na Mama Lishe wa mkoani humo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Rustika Turuka akipokea
madawati 90 kama sehemu ya mgao wa madawati hayo amewashukuru wadau na Mkuu wa
Mkoa kwa juhudi zao za kuwaunga mkono ili kufanikisha lengo la serikali la
kuhakikisha kuwa hakuna mwanafunzi wa shule ya msingi na sekondari anayekaa
chini.
Turuka
amesema kwa niaba ya wakurugenzi wote waliopokea madawati hayo watahakikisha wanayaelekeza
katika maeneo yenye upungufu na kusimamia yanatunzwa huku akiongeza kuwa
madawati hayo yataboresha mwandiko na
ufahamu wa wanafunzi hivyo kuinua kiwango cha ufaulu Mkoani Singida.
Akiwakilisha wadau
waliochangia madawati, Mkulima na Mfugaji Hassan Tati amesema kuwa Mkuu wa mkoa
wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amebuni njia nzuri ya kuwapa motisha kwa
kutoa Hati kwa wadau wote waliochangia jambo ambalo litaamsha ari zaidi katika
kuchangia shughuli za Maendeleo ya Mkoa na taifa kwa ujumla.
Tati amesema kuwa inasikitisha
sana pale anaposikia kuwa mkoa wa Singida unashika nafasi ya Tano kwa umasikini
katika Mikoa yote nchini ilihali ni mkoa wenye rutuba ya kutosha na eneo pana
katika uwekezaji hivyo amewasihi wananchi na wadau kwa pamoja kushirikiana kwa
pamoja katika kukomesha umasikini huo.
Mfanyabiashara Salum Nagji akipongezwa na kupewa hati ya shukrani kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe kama mdau mmojawapo aliyechangia madawati, anayesoma taarifa ni Mwenyekiti wa Kuratibu harambee ya madawati Elias Seng'ongo na katikati ni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dokta Angelina Lutambi.
Sehemu ya madawati yaliyochangwa na wadau mbalimbali wa maendeleo Mkoani Singida.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mathew Mtigumwe na kulia kwake ni Katibu Tawala Mkoa
wa Singida Dokta Angelina Lutambi wakiwa wameketi katika madawati na Wakuu wa Wilaya za Mkoani Singida, waliosimama ni wakurugenzi wa halmashauri za Wilaya ya Singida mara baada ya makabidhiano ya madawati.
No comments:
Post a Comment