Thursday, August 25, 2016

MKUU WA MKOA AAGIZA MIRADI INAYOFADHILIWA NA BENKI YA DUNIA IKAMILIKE KWA MUDA ULIOPANGWA.Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew Mtigumwe akisikiliza maelezo ya hali ya ujenzi wa mradi wa barabara.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhandisi Mathew J. Mtigumwe amefanya  ukaguzi wa miradi miwili ya ujenzi inayofadhiliwa na Benki ya Dunia yenye thamani ya shilingi Bilioni  6 na milioni 168 inayotekelezwa katika Manispaa ya Singuida.

Baada ya Ukaguzi huo Mhandisi Mtigumwe ametoa ufafanuzi pamoja na maelekezo kwa mkandarasi anayejenga miradi hiyo chini ya kampuni ya Hari singh & Sons limited ya Mjini Moshi kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa muda uliopangwa.
Aidha ameonyesha kufurahishwa na kasi ya ujenzi wa Stendi Mpya ya mabasi makubwa yaendayo mikoani ambao umefikia asilimia 40 na kueleza kuwa ana imani ujenzi huo utakamilika Mwezi Januari kama mkataba wa ujenzi huo unavyoeleza.

Mhandisi Mtigumwe amesema hajaridhishwa na Ujenzi wa Barabara  ya kilometa 1.8 inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka stand ya zamani hadi Misuna kutokana na ujenzi huo kufanyika kwa kusuasua.

Kutokana na kutoridhishwa huko Mhandisi Mtigumwe amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Singida Bravo Lyapembile Kizito kukutana na mhandishi mshauri na mkandarasi anayejenga Barabara hiyo ili wajadiliane na kuona namna barabara hiyo itajengwa ndani ya kipindi cha mkataba.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa Bravo amesema maagizo waliyopewa watayatekeleza na ndani ya siku saba watakaa kikao hicho ili mkandarasi huyo akamilishe miraadi hiyo kwa wakati.

Bravo amesema maagizo mengine ni kusafisha eneo la stendi ya zamani ambalo lina kifusi ambapo ameahidi kulisafisha ndani ya mwezi mmoja.

Ameongeza kuwa Manispaa ya Singida inatarajia kuanzia mwezi ujao kuainisha maeneo ya stendi maalum kwa ajili ya Bajaji, Piki piki na Magari sambamba na kuwaondoa wale wote wanaoegesha magari, bajaji na piki piki katika maeneo yasiyostahili kama vile eneo la sokoni.

Naye Mhandisi Mshauri wa Mradi huo Lucas Nyaki amesema wamepokea maelekezo ya Mkuu wa Mkoa na watampata taarifa ya namna watakavyoweza kukamilisha miradi hiyo kwa muda hasa mradi wa barabara ambao hakuridhishwa na ujenzi wake.
Mhandisi Mshauri Lucas Nyaki  akimfafanulia jambo Mkuu wa Mkoa wakati wa ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa barabra na stendi mpya ya Mkoa wa Singida inayofadhiliwa na benki ya dunia Manispaa ya Singida.
 Ujenzi wa Stendi Mpya ukiendelea.

No comments:

Post a Comment