Tuesday, October 21, 2014

TFDA YATOA MAFUNZO KWA WASINDIKAJI WADOGO WA VYAKULA MKOANI SINGIDA.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akifungua mafunzo kwa wasindikaji wadogo  wa vyakula Mkoani Singida.

Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) imetoa mafunzo ya siku mbili kwa wasindikaji wadogo wa vyakula Mkoani Singida, mafunzo ambayo yamefanyika katika ukumbi wa Roman Catholic, mwishoni mwa wiki.

Akifungua mafunzo hayo Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan amesema wasindikaji wadogo wanaweza kuongeza kipato chao endapo watatumia vizuri mafunzo hayo na kuweza kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Liana amesema katika wakati huu wa ushindani wa utandawazi na biashara huria wasindikaji wadogo wataweza kufanikiwa ikiwa watahakikisha bidhaa wanazozalisha zinakidhi vigezo vya ubora na usalama.

Ameongeza kuwa changamoto za wasindikaji wa wadogo wa vyakula Mkoani Singida ni pamoja na kutokuzingatia usafi, vifungashio hafifu na duni, kuhifadhi bidhaa maeneo ya wazi na yenye jua, kuzalisha na kuingiza bidhaa sokoni bila kufuata taratibu zilizowekwa.



Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka TFDA Lazaro Mwambole  akizungumza katika mafunzo kwa wasindikaji wadogo  wa vyakula Mkoani Singida.

Aidha Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka TFDA Lazaro Mwambole amesema mafunzo hayo ya siku mbili yamelenga kuwasaidia wasindikaji wadogo kukabiliana na changamoto zinazowakabili.

Mwambole amesema mafunzo yamejumuisha mada za kanuni za uzalishaji wa vyakula, usajili wa majengo ya vyakula, usajili wa vyakula na ukadiriaji wa muda wa matumizi wa vyakula vilivyofungashwa, kanuni na miongozo inayohusu usindikaji wa chakula salama pamoja na kuongeza kiwango cha uzingatiaji wa kanuni bora za uzalishaji wa vyakula.
 
Naye mmoja wa washiriki hao Bi. Amina Kisenge amesema mafunzo hayo yatawasaidia katika kukuza viwanda vyao, kuongeza ajira na kipato katika ngazi ya kaya, kukuza kilimo cha mazao ya chakula kutokana na uwepo wa soko la mazao ya vyakula hivyo.


























Wasindikaji wadogo wa vyakula Mkoani Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan.



























Baadhi ya wasindikaji wadogo wa vyakula Mkoani Singida wakisikiliza mada katika mafunzo yalioandaliwa na TFDA juu ya usindikaji wa vyakula.

No comments:

Post a Comment