Wednesday, August 20, 2014

HOSPITALI YA MKOA WA SINGIDA YAWA YA KWANZA KITAIFA KWA UBORA WA KUKINGA NA KUDHIBITI MAAMBUKIZO KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA.





Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid akijiandaa kukabidhi tunzo ya Ubora wa Kukinga na Kuthibiti Maambukizo katika Utoaji wa huduma za Afya kwa Mkoa wa Singida, Kushoto kwake ni Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Jhpiego Jeremy Zoungrana. 
 
Hospitali ya Mkoa wa Singida imepata tunzo ya Kitaifa  ya ubora wa Kukinga na Kudhibiti maambukizo katika utoaji wa huduma za afya, tunzo ambayo imekabidhiwa jana na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid.

Tunzo hiyo imeratibiwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa jamii kwa kushirikiana na Shirika lisilo la Kiserikali la Jhpiego, na Mfuko wa Dharura wa Rais wa Msaada kuhusu Ukimwi (PEPFAR)  kupitia kituo cha kuzuia na kupambana na Magonjwa (CDC) na kukabidhiwa kwa Mwenyekiti wa Kitengo cha Uhakiki wa Huduma za Afya wa Hospitali hiyo Dokta Abdalah Bala.

Katika hafla ya kukabidhi tunzo hiyo, Dokta Rashid ameitaka  hospitali ya Mkoa wa Singida kuhakikisha kuwa ubora huo haushuki bali unaongezeka huku akiipongeza kwa kuwa hospitali ya kwanza Tanzania kwa kupata tunzo hiyo.


Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid 

Aidha Dokta Rashid ameutaka uongozi wa Hospitali kuhakikisha kuwa asilimia 50 ya mapato ya makusanyo inaelekezwa "Medical Stores Department" MSD ili kuwezesha hospitali hiyo kuwa na uhakika wa kupata dawa.

Ameongeza kuwa kiwango kilichofikiwa na ospitali hiyo ni cha kupongezwa na kiwe mfano kwa hospitali nyingine ili ziweze kujifunza na kuongeza ubora wa kukinga na kudhibiti maambukizi katika utoaji wa huduma za afya.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid akizungumza na waatumishi wa idara ya afya katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
 
Naye Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la  Jhpiego Jeremy Zoungrana amesema mpango wa kuzua na kukinga maambukizo katika utoaji wa huduma ni wa manufaa makubwa sana hasa katika kipindi hiki ambacho kuna magonjwa ya Mlipuko kama Ebola.

Zoungrana ameahidi ushirikiano na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hasa  katika kusaidia hospitali zinazoonyesha bidii na kujituma kama hospitali ya Mkoa wa Singida.




Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la  Jhpiego, Jeremy Zoungrana akisoma hotuba yake wakati wa utoaji wa tunzo hizo.

Kwa upande wake Katibu Tawala Msaidizi Idara ya Afya na Ustawi wa Jamii Mkoa wa Singida Dokta Dorothy Kijughu Gwajima amesema ushindi wa hospitali ya Mkoa wa Singida umetokana na juhudi na kujitoa kwa watumishi wa Idara hiyo Mkoani hapa.

Dokta Gwajima amesema atahakikisha ubora wa huduma za hospitali ya Mkoa wa Singida unaendelezwa kwa kuwa tunzo hiyo itawajengea uwezo wa kujiamini  na kuendelea kutoa huduma katika ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa.

Watumishi wa Idara ya Afya kutoka Hospitali ya Mkoa wa Singida wakiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii Dokta Seif Rashid mara baada ya kupokea tunzo.



























Mwenyekiti wa Kitengo cha Uhakiki wa Huduma za Afya wa Hospitali hiyo Dokta Abdalah Bala akifurahia tunzo ya hospitali ya Mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment