Friday, August 22, 2014

WATU WAWILI WAPOTEZA MAISHA NA WENGINE 33 KUJERUHIWA KATIKA AJALI YA BASI MKOANI SINGIDA.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dk. Parseko Vicent Kone.
Watu wawili wamepoteza maisha na wengine 33 kujeruhiwa katika Kijiji cha Nkuhi,wilaya ya Ikungi, mkoani Singida baada ya basi la Kampuni ya KISBO SAFARY lililokuwa likitokea Dar-es-Salaam kwenda Kahama kupasuka gurudumu la mbele na kisha kupinduka mara tatu.
 
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Singida, Dk.Deogratius Banuba amethibitisha kupokea majeruhi na maiti hao na kuongeza kuwa kati ya majeruhi hao kumi wamevunjika mifupa.
 
Aidha, mmoja kati ya  majeruhi waliolazwa wodi namba tatu katika Hospitali hiyo, Bi Wilhelimina Stephano amesema tangu walipofika Chalinze basi hilo lilianza kusumbua kama vile kuna kitu kama mpira uliokuwa ukiungua.
 
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk.Parseko V. Kone ameonyesha  masikitiko yake kutokana na ajali hiyo na kukemea tabia ya baadhi ya madereva wanaokwenda mwendo kasi unaosababisha ajali na vifo vya abiria.

No comments:

Post a Comment