Tuesday, June 17, 2014

WATOTO MKOANI SINGIDA WAUNGANA NA WENZAO AFRIKA KUADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA.



Wanafunzi wa shule ya Msingi Kinyambuli wakiandamana mbele ya Mgeni rasmi Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Mwl. Queen M. Mlozi.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Mwl. Queen M. Mlozi amesema hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wazazi walioshindwa kuwapeleka shule watoto wanne mwaka 2011 na wawili mwaka 2012 waliofaulu kujiunga na masomo ya sekondari Wilayani Mkalama.

Mlozi ametoa agizo hilo jana wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ambapo Mkoani Singida maadhimisho hayo yamefanyika katika kijiji cha Kinyambuli, Tarafa ya Kirumi, Wilaya ya Mkalama.

Amesema watoto wanapaswa kupata haki zote ikiwa ni pamoja na wazazi wote kuhakikisha watoto walio chini ya umri wa miaka mitano wanapewa chanjo zote kabla ya umri wa chanjo hizo kupita.

Mlozi amepokea maandamo ya watoto wa Shule ya Msingi Kinyambuli na Kushiriki katika zoezi la kutoa chanjo ya Matone ya Vitamini A kwa baadhi ya watoto kijijini hapo.

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Queen M. Mlozi akitoa chanjo ya Matone ya Vitamini A kwa moja ya mtoto katika kijiji cha Kinyambuli, Wilayani Mkalama.
Naye Mwenyekiti wa Kitongoji cha Wahadzabe cha Kibamba, Munguli, Bw. Edward Mashimba amepokea msaada wa chakula kwa ajili ya jamii hiyo  na kuongeza kuwa jamii hiyo imezoea kula matunda, mizizi na nyama.
Mashimba ameongeza kuwa watoto wa jamii hiyo pamoja na wazazi wameona umuhimu wa elimu na wamewapeleka shule pia wamekubali kutumia dawa za hospitali tofauti na zamani ambapo walikuwa wakitumia mitishamba.


Mwenyekiti wa Kitongoji cha Wahadzabe cha Kibamba, Munguli, Bw. Edward Mashimba akipokea Msaada wa chakula kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Mwl.Queen M. Mlozi.

Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka 2014 ni "Kupata Elimu bora na isiyo na Vikwazo ni haki ya kila mtoto".
 


Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Mwl.Queen M. Mlozi akipiga mpira kuashiria kuanza kwa mashindano ya mpira wa miguu katika maadhimisho hayo.



Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Singida Mwl.Queen M. Mlozi akicheza muziki na wanafunzi wa shule ya msingi Kinyambuli katika maadhimisho hayo.

No comments:

Post a Comment