Saturday, June 28, 2014

KATIBU MKUU KIONGOZI BALOZI OMBENI Y. SEFUE AFANYA ZIARA YA KIHISTORIA MKOANI SINGIDA.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y Sefue akitoka nje ya jengo jipya la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida, Kushoto kwake ameambatana na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan na Kulia kwake ni Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI Jumanne A. Sagini.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y. Sefue jana amefanya ziara ya kikazi Mkoani Singida akiwa ni Katibu Mkuu Kiongozi wa kwanza kufanya ziara Mkoani Singida kwa kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Balozi Sefue ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Sekretarieti za Mikoa (OWM-TAMISEMI) Jumanne A. Sagini, Wakurugenzi kutoka TAMISEMI na Watendaji wa Ofisi ya Rais Ikulu.

Balozi Sefue amezungumza na watumishi wa umma Mkoani Singida pamoja na kupata taarifa mbalimbali za Utekelezaji wa majukumu ya Sekretarieti ya Mkoa na Halmashauri ya Mji wa Singida pamoja na Taasisi nyingine za Umma Mkoani hapa.

Amesema watumishi wa umma wanapaswa kutii sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ili waweze kutenda haki na kutekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Amewaasa watumishi wa umma kuongeza uadilifu baina yao wenyewe na katika kuwahudumia wananchi ili kupunguza malalamiko na kuongeza utii wa sheria kwa wananchi.

Balozi Sefue amewapongeza watumishi wa umma Mkoa wa Singida kwa bidii katika utendaji kazi na kuongeza kuwa mafanikio yalioonekana katika Hospitali ya Mkoa wa Singida yanadhihirisha uadilifu wa watumishi Mkoani hapa.

Amesema tuzo mbalimbali zilizotolewa kwa hospitali ya Mkoa kutoka taasisi mbalimbali zinadhihirisha kiwango kizuri cha utoaji huduma wa sekta ya Afya Mkoani Singida hasa afya ya mama na mtoto.

Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y Sefue akitazama moja ya Tuzo za Hospitali ya Mkoa wa Singida.


Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y Sefue na Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI Jumanne A. Sagini wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Hospitali ya Mkoa, hapo mezani ni tuzo mbalimbali za mafanikio ya  Hospitali ya Mkoa wa Singida.

Balozi Sefue amewataka watendaji na viongozi Mkoani Singida kuhakikisha kuwa watumishi wanakuwa na mazingira mazuri ya utendaji kazi ili kufanikisha ufanisi katika kumhudumia wananchi.
 
Ameongeza kuwa juhudi za kuwaendeleza watumishi ziongezwe pamoja kusimamia stahili za watumishi wa umma kama kupandishwa vyeo na kuongezewa ujuzi kwa kozi, mafunzo na semina mbalimbali.

Kwa upande wao watumishi Mkoani Singida wamefurahishwa na ziara ya Balozi Sefue na kuongeza kuwa wafanyakazi wanapenda kupata motisha kutoka kwa waajiri wao si tu motisha ya pesa bali hata kuhakikisha mazingira mazuri ya utendaji wao wa kazi.

Wameongeza kuwa ujio wa Balozi Sefue umewatia moyo na kuona kuwa serikali inatambua na kuthamini utendaji wao wa kazi licha ya changamoto ya ufinyu wa bajeti, vitendea kazi na watumishi.


























Kaimu Mhasibu Mkuu ofisi ya RAS Singida Melkior Rweyemamu akimshukuru na kumpongeza Balozi Sefue kwa kuutembelea Mkoa wa Singida na kuzungumza na watumishi wa Umma.


























Balozi Sefue na ujumbe alioambatana nao wakitazama vifaa katika hospitali mpya ya Rufaa ya Mkoa wa Singida.


























Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Ombeni Y Sefue,  Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan na Katibu Mkuu OWM-TAMISEMI Jumanne A. Sagini wakiwa katika picha ya pamoja na viongoz, watumishi na watendaji mbalimbali wa Mkoa wa Singida.

No comments:

Post a Comment