Tuesday, August 05, 2014

MKUTANO WA WARATIBU WA UKIMWI KANDA YA KATI WAANZA RASMI.






Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na waratibu wa Ukimwi Kanda ya Kati, Kulia kwake ni Mratibu wa Ukimwi Manispaa ya Singida Anna Churi na kushoto ni Mratibu wa TACAIDS Mkoa wa Singida Fedes Mdalla.

Mkutano wa Waratibu wa Ukimwi Kanda ya Kati inayojumuisha Mikoa ya Dodoma, Singida, Tabora na Kigoma kwa mwaka 2014 umefunguliwa rasmi leo Mkoani Singida na Katibu Tawala Mkoa  Liana Hassan.

Hassan amewaasa waratibu kuzingatia maazimio watakayofikia katika mkutano huo ili wasiishie tu kupanga bali ni lazma kuyatekeleza na kuhakikisha taarifa zinazohusu Ukimwi zinatolewa kwa wakati.

Amesisitiza umuhimu wa waratibu hao kukutana mara moja kila mwaka kujadili mambo yanayohusu kada yao katika kanda hiyo  na kupongeza hatua ya kufanya mikutano hiyo  ndani ya kanda kuliko nje ya nchi kwani kutaongeza garama ya mikutano hiyo.

Hassan amewataka waratibu wa Ukimwi kuhakikisha pesa inayotengwa na Mikoa na halmashauri zao kwa ajili ya mapambano dhidi ya Ukimwi inapatikana na kutumika kulingana na malengo yaliyowekwa.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akifungua mkutano wa waratibu wa Ukimwi Kanda ya Kati leo asubuhi.

Amesema takwimu zinaonyesha  maambuki ya Virusi vya Ukimwi (VVU) Mkoa wa Singida yameongezea kutoka asilimia 2.7 ya mwaka 2013 hadi kufikia asilimia 3.2 kwa mwaka 2014.

Hassan amesema takwimu hizo zinaweza kuwa ni ishara ya kuwa elimu imewafikia wananchi na wamejitokeza kwa wingi kupima pia inaweza kuwa ishara ya upatikanaji wa takwimu sahihi za maambukizi ya VVU Mkoa wa Singida.

Naye Mratibu wa Tume ya Kupambana na Ukimwi (TACAIDS) Mkoa wa Singida Fedes Mdala ameushukuru uongozi wa Mkoa kwa kuweka kipaumbele mapambano dhidi ya Ukimwi.

Mratibu wa TACAIDS Mkoa wa Singida Fedes Mdalla (katikati) akifurahia jambo na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan (kushoto kwake) pamoja na Mratibu wa Ukimwi Mkoa wa Singida Patric Kassango.

Mdala amempongeza Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan kwa kutenga asilimia 3 ya pesa ya matumizi ya kawaida (OC) kila mwezi kusaidia watumishi wanaoishi na VVU.

Ameongeza kuwa Mkoa uko katika hatua nzuri ya kuandaa Mpango Mkakati wa kupambana na Virusi vya Ukimwi ambao utasaidia katika kupambana na VVU.

Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Ikungi Haika Massawe amesema mkutano huo utawasidia kubadilishana uzoefu, changamoto na mafanikio katika kada yao.

Mratibu wa Ukimwi Halmashauri ya Ikungi Haika Massawe akihojiwa na mwandishi wa Standard Radio Iman Msigwa (hayupo pichani) kuhusu mkutano wa waratibu wa Ukimwi Kanda ya Kati.

Massawe amesema changamoto kubwa wanayokutana nayo ni unyanyapaa unaowafanya waathirika wengi wa VVU kufanya siri hali yao hivyo kupeleka kasi ya maambukizi kuongezeka.

Ameongeza kuwa elimu juu ya VVU na Ukimwi imetolewa ya kutosha isipokuwa wananchi bado ni wagumu kubadili tabia hatarishi.


Katibu Tawala Mkoa wa Singida Liana Hassan akizungumza na waratibu wa Ukimwi Kanda ya Kati leo asubuhi.

No comments:

Post a Comment