Mkuu wa Mkoa
wa Singida Mhe. Halima Dendego, amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri Saba za
mkoa huo kuhakikisha wanafanya ukaguzi wa haraka kwenye shule za Msingi na Sekondari
ili kujua hali ya uhaba wa madawati ilivyo na kuchukua hatua ya kuondoa tatizo
la Wanafunzi kujisomea wakiwa wamekaa sakafuni haraka iwezekanavyo.
Mheshimiwa Halima
Dendego ametoa kauli hiyo leo (24 Mei, 2024) wakati akizungumza na Viongozi wa
Manispaa ya Singida na Walimu wa shule ya Msingi Bomani iliyopo Manispaa ya
Singida baada ya kufanya ziara ya kustukiza kwenye shule hiyo kufutia kusambaa
kwa picha mbalimbali kwenye mitandao ya kijamii zikionyesha wanafunzi wa shule
hiyo wakifanya mtihani yao wakiwa wamekaa chini.
RC Dendego, amesema picha hizo zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zimesababisha taharuki kubwa kwa jamii tofauti na hali ilivyo kwenye shule hiyo ambayo inaupungufu wa madawati Nane (8).
Mkuu huyo wa
mkoa wa Singida pia ametoa siku Saba (7) kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida
kuhakikisha anapeleka madawati Nane yanayohitajika kwenye shule hiyo ili
wanafunzi wa shule hiyo ya Bomani waweze kujifunza na kujisomea katika hali
bora na nzuri zaidi.
Naye, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Bomani Joachim Msechu, amesema sio kweli kuwa shule hiyo inaupungufu mkubwa wa madawati na upungufu uliopo ni madawati Nane tu na walikuwa kwenye mchakato wa kukarabati madawati mengine yaliyoharibika ili wanafunzi waweze kuyatumia.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida Mhe. Godwin Gondwe,
amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo kuwa maelekezo aliyoyatoa watayafanyia kazi
kuanzia sasa ili kuondoa mapungufu madogo madogo yanayotokea kwenye sekta ya
elimu ili kuimarisha shughuli za ufundishaji wa wanafunzi mashuleni.
Kwa sasa shule ya msingi Bomani iliyopo katika Manispaa ya
Singida ina wanafunzi 894 na walimu 16.
MATUKIO KATIKA PICHA
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (wapili kutoka kushoto) akiwasalimia wanafunzi wa shule ya Msingi Bomani wakati wa ziara hiyo. Mei 24, 2024.
No comments:
Post a Comment