Sunday, February 05, 2023

Bilioni 7.562 kutumika kuchimba visima sita Mkoani Singida.

 

Wakala wa Usambazaji wa maji Safi na usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) wamesaini mikataba sita (6) yenye thamani ya Tsh. Bilion 7.56 ambayo inahusu uchimbaji wa visima katika Wilaya mbalimbali za Mkoa wa Singida ili kupunguza tatizo la upatikanaji wa  maji mijini na Vijijini.

Akiongea kabla ya utoaji saini mikataba hiyo hafla iliyofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa huo Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba amewataka mameneja wa RUWASA wa Mkoa na Wilaya kusimamia zoezi hilo la uchimbaji visima kikamilifu ili kulinda thamani ya fedha zitakazotewa.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo wakati wa hafla ya usainishaji wa mikataba ya miradi ya maji mkoani Singida.

Aidha amewaagiza mameneja wa Wilaya na Mkoa wakiona Mradi wowote kati ya hiyo unasuasua  wahakikishe wanamchukulia hatua kali za kisheria Mkandarasi husika ili kutoa funzo kwa wengine na kuhakikisha thamani ya fedha inasimamiwa.

Hata hivyo amewataka wahandisi hao kusimamia kikamilifu maelekezo (Specification) ili pindi miradi ikamilike kwa ubora wake  na iwe na tija iliyokusudiwa.

"Hatutahitaji kazi inakamilika ndani ya miezi mitatu tunaambiwa maji hayatoki au tanki lina matatizo naomba tusimamie viwango "specifications" Serukamba.

RC Serukamba amesema endapo miradi hiyo ikikamilika katika viwango vilivyokusudiwa anaamini kwamba upatikanaji wa maji Vijijini utakuwa umefikia au umekaribia asilimia 85 na Mijini kwa asilimia 95.

"Tunataka tuache kuonge habari ya maji endepo miradi yetu ukikamilika tutaondoa tatizo la upatikanaji maji mijini na Vijiji" Serukamba

Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida Martha Mlata amesema Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali hivyo ni jukumu la kila kiongozi kuhakikisha kwamba unatekelezwa kwa usahihi na kwa wakati.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Singida Martha Mlata akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Akizungumzia kuhusu utekelezaji wa Ilani ya CCM Mlata, ameeleza kwamba Mkoa wa Singida umeendelea kutekeleza miradi kwa viwango ambapo ameeleza kwamba kwenye miradi ya maji itawasaidia kumtua mama ndoo ya maji kichwani.

Kwa upande wake Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said,  amesema miradi hiyo itatekelezwa na makampuni ya wazawa ambapo amesema kila Wilaya itakuwa na mradi mmoja.

Mhandisi Lucas Said  ameeleza kwamba miradi hiyo ikikamilika itaweza kuhudumia idadi ya watu wapatao 77,769 katika maeneo mbalimbali Mkoani hapo.

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Singida Mhandisi Lucas Said, akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Wakulima watakiwa kuacha kulima kwenye hifadhi ya barabara

 

Wakulima Wilayani Ikungi wamelalamikiwa kwa kitendo cha kulima katika maeneo mengi ya hifadhi ya Barabara jambo ambalo linakwamisha jitihada za matengenezo ya Barabara hasa nyakati hizi za mvua.

Lalamiko hilo limetolewa hivi karibuni na Meneja wa TARURA Wilaya ya Ikungi Mhandisi Ally Number wakati wa majadiliano yaliyofanyika katika Kikao cha Baraza la Madiwani kilichofanyika hivi karibuni katika Halmashauri hiyo.

Mhandisi Ally amebainisha kwamba wakulima wengi Katika kata za Sepuka Makilawa Ihanja Nduru Mkiwa na Mwaru wamelima Katika hifadhi ya Barabara Jambo ambalo litasababisha kucheleweshewa kwa kazi za matengenezo ya Barabara.

Sambamba na hilo Mhandisi Ally amesema bado wafugaji wa Wilaya hiyo wanaendelea kupitisha mifugo Barabarani Jambo ambalo kunasababisha uharibifu mkubwa wa barabara hasa kipindi hiki cha mvua hivyo kuiomba jamii kuacha tabia hiyo kwa kuwa Barabara hizo hutumia fedha nyingi za Serikali katika kukarabatiwa.

Awali Baraza la Madiwani lilipitisha bajeti ya Tarura Ikungi kwa mwaka 2022/23   kiasi cha Bilioni 4.72 Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Ally Juma Mwanga alisema endapo zikitumika kama mipango ilivyowekwa wanategemea maeneo mengi yatafunguliwa na barabara nyingi zitapitika.

Mwenyekiti huyo amesema Kata zote za Ikungi zitaguswa katika bajeti hiyo ambayo yapo maeneo ya kata hizo yatajengwa madaraja kata nyingine Barabara zitafunguliwa mpya wakati maeneo mengine yakijengwa madaraja makubwa na madogo.

Hata hivyo Mhandisi Ally alitoa ufafanuzi kwamba fedha hizo zilizotengwa zitatumika katika utenegenezaji wa barabara Madara na nyingine kwa ajili ya usimamizi ambapo jumla ya KM 156 na madaraja 20 na makalavati 61 vitajengwa.


Friday, February 03, 2023

Serukamba amaliza mgogoro wa ardhi uliodumu kwa miaka zaidi ya 30.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewataka wananchi wa Mkoa huo kufuata taratibu za upimaji wa ardhi na kuzimiliki kihalali ili kupunguza migogoro ya ardhi katika jamii.

Kauli hiyo ameitoa leo tarehe 3/02/2023 wakati akitatua mgogoro wa mpaka uliodumu kwa miaka 30 katika eneo la ukubwa wa ekari 132 lililopo katika kijiji cha Kititimo kata ya Mungu maji katika Manispaa ya Singida.

Eneo hilo ambalo limetajwa kumilikiwa kisheria na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) tangu mwaka 1945 lilivamiwa na wananchi ambao wakijenga na wangine kufanya shughuli za kilimo.

Hata hivyo RC Serukamba amewatoa wasiwasi wananchi wenye makazi katika eneo hilo kwa kipindi kisichopungua miaka 12 kwamba hataondolewa katika maeneo yao na kuagiza Halmashauri kuwapimia ili waweze kumilikishwa kihalali huku akieleza kwamba mashamba yote yatabaki katika umiliki wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Amewataka wananchi kujenga tabia ya kumiliki maeneo (ardhi) kisheria badala ya kufanya uvamizi jambo ambalo litakuwa likiwasababishia hasara kila mara.

"Tuache tabia ya kuvamia maeneo ya watu itakusababishia hasara na ukiwa na eneo lako hakikisha linapimwa ili ulimiliki kisheria" Serukamba.

Aidha Serukamba ametoa onyo kali kwa wananchi wa Kititimo kwamba isije ikatokea mtu yeyote akang'oa "Bikoni" zilizowekwa kwa kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA


Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kushoto) akimsikiliza moja ya Mzee wa eneo lililokuwa na mgogoro.
Zoezi la upimaji na uwekaji bikoni likiendelea katika eneo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akisisitiza jambo kwa wakazi wanaolizunguka eneo hilo lililokuwa na mgogoro.


Wednesday, February 01, 2023

Mahakimu Mkoani Singida wakumbushwa kuwatendea haki Wananchi.

 

Mahakimu na Wasimamizi wa Sheria Mkoani Singida wametakiwa kuepuka vitendo vya kupokea rushwa ambayo unaosababishwa upindishwaji wa Sheria ili kuwatendea haki wananchi huku wakihimizwa  kusaidia kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Maelezo hayo yametolea leo na Jaji Mstaafu Fatuma Massengi wakati wa kilele cha wiki wa Sheria inayoadhimishwa kila tarehe 1 Februari Nchini, maadhimisho ambayo Mkoa wa Singida zimeadhimishwa katika viwanja vya Mahakama ya Mkoa iliyopo mjini Singida.

Jaji Massengi amesema katika vitabu vya dini vimeeleza kwamba Mahakimu watakuwa wa mwisho kuingia mbinguni kwa kuwa maswali yatakuwa mengi hasa kwa wale ambao hawakuwatendea haki wanaanchi.

Aidha amewaasa Mahakimu kutenda haki na kusimamia Sheria kwa kuwa kazi hiyo ni kazi ya Mungu na ni msingi wa Maendeleo ya nchi ambapo kama Sheria itapindishwa itasababisha kudumaza uchumi wa nchi.

"Tuache kupokea rushwa kwa kuwa inadidimiza uchumi, napenda kuwakumbusha Mahakimu kuhakikisha wanatenda kazi ya Mungu bila upendeleo, vitabu vya dini vinaeleza kwamba Mahakimu watakuwa wa mwisho kuingia mbinguni kwa kuwa watakuwa na maswali mengi ya kujibu" Alisema Jaji Fatuma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewaomba wanasheria wa Serikali na Binafsi kuambatana naye kila wiki ya tatu ya kila mwezi kwenda Wilayani kutatua kero za Wananchi badala ya kusubiri maofisini.

Aidha amewataka Maafisa wa Mahakama kuongeza jitihada ya kutoa elimu kwa wananchi ambao hawajui umuhimu wa kutatua migogoro yao nje ya Mahakama ili kuwapunguzia gharama kupeleka mashtaka Mahakamani ambayo yangeweza kutafutiwa kwa usuluhishi.

"Tumeanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi walipo kwenda kusikiza changamoto zinazowakabili hivyo niwaombe mawakili wa Serikali na Binafsi tuwe tunaambatana kwenda kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi walipo wananchi". Serukamba

Hata hivyo amepongeza Mahakama kwa kuwa mabingwa wa kutumia teknolojia ya Habari kutatua kuendesha mashtaka na kupunguza mrundikano wa kesi katika Mahakama zao.

Naye Hakimu mkazi wa Mahakama kuu ya Singida Allu Nzowa amesema Mahakama imejipanga kuhakisha kwamba katika mwaka mpya wa Sheria watahakikisha haki za watu zinapatikana kwa wakati.

Nzowa amewataka wananchi kuepuka migogoro kwa sababu imekuwa chanzo cha kudidimiza uchumi kwa wananchi na kuleta umaskini kwakuwa watu wanashindwa kuendelea kuzalisha au kufanya biashara kwa sababu ya migogoro.

Awali Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida  Juma Hasani Salige alieleza kwamba wananchi wanapata changamoto kuendesha migogoro kwa gharama kubwa huku ikisababisha kupungua na kudhoofika kwa uchumi wao, huku mwakilishi wa Chama cha Mawakili wa kujitegemea (LLS) Salma Musa,  aliomba wanasheria binafsi washirikishwe kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na kupatiwa jengo la ofisi Mkoani hapa.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA

Tuesday, January 31, 2023

RAS SINGIDA ATAKA MRADI WA SHULE BORA UTENGENEZE MFUMO WA KUTOA MAFUNZO KWA WALIMU

KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, ameuagiza Mradi wa Shule Bora unaotekelezwa katika mikoa tisa (9) nchini kutengeneza mfumo wa kutoa mafunzo kwa walimu wa Mkoa wa Singida ili kuinua viwango vya elimu mkoani hapa.

Akifungua mkutano wa uhamasishaji wa Programu ya Shule Bora kwa wasimamizi na wahariri wa vyombo vya habari leo, amesema walimu watakaopewa mafunzo hayo nao watakwenda kuwafundisha wenzao.

"Kila Halmashauri kuwe na 'trainers' ambapo kutatafutwa 'centre'  walimu watakuwa wanakutana na hivyo wataguswa walimu wengi kwa wakati mmoja na mpango huu uanze mara moja mwezi Februari mwaka huu," amesema.

Mradi wa Shule Bora umelenga kuiunga mkono Serikali ya Tanzania katika kuinua kiwango cha elimu jumuishi pamoja na kuweka mazingira salama ya kujifunzia kwa wanafunzi wa kike na kiume katika shule za Serikali zilizopo katika mikoa ya  Singida, Dodoma, Simiyu, Tanga, Mara, Rukwa, Katavi, Pwani na mkoa wa Kigoma.


Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoani Singida Samweli Daniel, akitoa taarifa ya Mradi wakati wa mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Afisa Elimu Mkoa wa Singida Maria Lyimo, akizungumza wakati wa mkutano huo.


Meneja Mawasiliano wa Shule Bora Bw. Raymond Kanyambo, akizungumza wakati wa Mkutano huo.

Mwandishi wa Habari Seif Takaza akizungumza wakati wa mkutano huo.
Saturday, January 28, 2023

Madereva kujengewa Ofisi.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba jana 27.01.2023  ameweka rasmi jiwe la msingi katika ujenzi wa Ofisi ya madereva Mkoani hapo  linalotarajiwa kugharimu zaidi ya Tsh. Milioni 79.6.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba (kulia) akiweka jiwe la msingi ujenzi wa Ofisi ya Madereva katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.

Akiongea na Watumishi baada ya kuweka jiwe hilo RC Serukamba amempongeza Katibu Tawala wa Mkoa huo Dorothy Mwaluko kwa kuleta wazo la kuwajengea Ofisi madereva ili waweze kujikinga na mvua jua na baridi jambo ambalo ameeleza kwamba litaleta ufanisi katika kazi yao.

RC amesema maamuzi hayo ni ya kijasiri kwakuwa Ofisi nyingi za Serikali hazina Ofisi maalum  za madereva hivyo akawataka madereva hao kutunza Ofisi hiyo na kuhakikisha kwamba wanafanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Katika hatua nyingine ameupongeza mpango wa kuwa na sare maalumu inayovaliwa siku ya Ijumaa huku akiueleza  kwamba inaonesha umoja katika kazi.

Amesema umoja huo utumike katika ufanyaji kazi kwa umahiri juhudi na maarifa na kila Mtumishi ahakikishe kwa nafasi yake anatatua changamoto za wananchi.

"Utanashati huu nilio uona usiwe wa siku ya Ijumaa pekee bali tujitahidi siku zote tupendeze, mtu mtanashati hata kazi zake anazifanya vizuri" Serukamba.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa huo Dorothy Mwaluko amemueleza RC Serukamba kwamba ujenzi wa ofisi hiyo ni sehemu ya majengo mbalimbali yanayoendelea kujengwa na ofisi hiyo yakihusisha nyumba za Maafisa Tarafa ambazo nazo atakaribishwa kuzizindua siku chache zijazo.

Aidha akiongea na Watumishi hao Mwaluko amewataka  kuongeza juhudi katika kufanya kazi na kuacha mazoea katika kazi  ili kuwasaidia wananchi wa Singida huku akikemea swala la utoro kazini.

Awali akitoa taarifa ya awali Mhandisi wa Mkoa Domicianus Kirina amesema ujenzi wa ofisi hiyo ulianza tarehe 19 Desemba, 2022 ambapo inategemewa  kukamilika tarehe 1 Machi, 2023.

Ameleeza kwamba katika kufanikisha zoezi hilo ziliundwa kamati nne ambazo ni kamati ya manunuzi, mapokezi, ulinzi na kamati ya ufuatiliaji.

Mhandisi Domicianus  amesema fedha ambazo zimekwisha tumika zilikuwa ni Tsh. Milioni 56.04 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa mbalimbali na malipo ya fundi.

Mwisho.