"WATOTO WANAOPATA LISHE WANAFABYA VIZURI DARASANI" MWL. DULENGA
Wazazi na walimu wameaswa kudumisha ushirikiano wa karibu ili kuhakikisha
elimu bora inaendelea kutolewa shuleni na kuleta matokeo chanya kitaaluma. Rai
hiyo imetolewa leo tarehe 12 Februari 2026 na Afisa Elimu Mkoa wa Singida, Bw.
Makwasa Dulenga, wakati akishiriki mahafali ya kidato cha sita yaliyofanyika
katika Shule ya Sekondari Ndago mkoani Singida.
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Makwasa amesema mafanikio ya kitaaluma shuleni yanategemea mshikamano wa wadau wote wa elimu, hususan wazazi na walimu wenyewe. Amefafanua kuwa ushirikiano huo hujidhihirisha kupitia hatua mbalimbali ikiwemo uhamasishaji wa utoaji wa chakula shuleni, ufuatiliaji wa maendeleo ya wanafunzi na michango ya hiari inayowawezesha walimu wanaojitolea kuendelea kutoa huduma bora ya ufundishaji.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao wanapata lishe bora
wakiwa shuleni, kwa kuwahimiza kuchangia chakula shuleni akisisitiza kuwa kuna
uhusiano wa moja kwa moja kati ya lishe bora na ufaulu mzuri darasani. Amesema
mwanafunzi anayepata chakula chenye virutubisho muhimu shuleni huwa na uwezo
mkubwa wa kuzingatia masomo na kufanya vizuri katika mitihani.
Vilevile, Afisa Elimu amewahimiza wanafunzi kuendelea kuthamini fursa ya
elimu kwa kujituma zaidi katika masomo yao, akibainisha kuwa wazazi na walezi
wao wanajitoa kwa hali na mali kuhakikisha wanawapatia mahitaji muhimu ya shule
ikiwemo sare na vifaa vya kujifunzia ili kuwajengea msingi bora wa maisha ya
baadaye.
Awali akiwasilisha taarifa fupi ya shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Ndago, Bi. Prisca T. Msemo, amesema wanafunzi wa kidato cha sita wanaohitimu wameonyesha kiwango kizuri cha maandalizi kitaaluma kupitia mitihani mbalimbali ya majaribio waliyoifanya, ikiwemo mtihani wa utimilifu (Mock) wa Mkoa wa Singida. Ameeleza kuwa katika matokeo ya mtihani huo, shule ilishika nafasi ya tano kati ya shule 27 za mkoa, ambapo wanafunzi 54 walipata daraja la kwanza, wanafunzi 13 daraja la pili na mwanafunzi mmoja daraja la tatu, matokeo ambayo yanaonesha juhudi za walimu na wanafunzi pamoja na mazingira mazuri ya ufundishaji na ujifunzaji yaliyopo shuleni hapo.
Kwa upande wa baadhi ya wazazi waliohudhuria mahafali hayo wameipongeza hotuba ya mgeni rasmi na kuahidi kuendeleza ushirikiano katika malezi na elimu ya watoto wao. Wamesema wataendelea kuhakikisha wanafunzi wanapata mazingira mazuri ya kusoma ili waweze kufikia ndoto zao za kuendelea na masomo ya ngazi za juu. "Mgeni rasmi umesema maneno mazuri sana, umewahusia vijana wetu na sisi wazazi umetuhusia, basi tutashirikiana na walimu wetu. Pia nawashukuru walimu kwa kuwalea watoto wetu na ninyi watoto wetu bado kuna hatua huko mbele hivyo jitahidini katika masomo yenu sisi tuko pamoja na walimu wenu." Amesema mmoja katika wazazi.
Nao wanafunzi wa kidato cha sita wa Shule hiyo wamewashukuru walimu wao kwa
malezi bora ya kitaaluma na kimaadili waliyoyapata katika kipindi chote cha
masomo yao shuleni hapo. Wamesema juhudi, moyo wa kujitolea na ufuatiliaji wa
karibu kutoka kwa walimu wao umekuwa chachu ya maendeleo yao darasani na nje ya
darasa. Aidha, wameahidi kuwa watajituma kwa bidii katika mitihani yao ya
mwisho ili kufanya vizuri zaidi na kuendeleza rekodi ya ufaulu wa shule hiyo,
huku wakisisitiza kuwa wataendelea kuitunza heshima ya shule yao kwa matokeo
mazuri yatakayodhihirisha ubora wa elimu waliyoipata.
No comments:
Post a Comment