Monday, June 29, 2026

BAJETI YA 2026/2027 NI SILAHA YA KUPAMBANA NA UTAPIAMLO SINGIDA



  Katika kuhakikisha Mkoa wa Singida unaendelea kupiga hatua katika kupunguza utapiamlo na kuimarisha afya ya jamii kama msingi wa maendeleo endelevu, Kamati ya Lishe ya Mkoa imeelekeza kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 iwe chombo cha msingi cha kuimarisha utekelezaji wa afua za lishe kwa matokeo yanayopimika.



Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida na Mwenyekiti wa Kamati ya Lishe ya Mkoa, Dkt. Fatuma Mganga, ameitaka Serikali na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inatoa kipaumbele kwa afua za lishe, akisisitiza kuwa vita dhidi ya utapiamlo haviwezi kushindwa bila uwekezaji wa makusudi katika mipango na matumizi ya fedha.



Akifungua kikao cha Kamati ya Lishe ya Mkoa wa Singida cha robo ya Januari–Machi 2026 kilichofanyika Juni 30, 2026 katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Dkt. Mganga amesema lishe si suala la sekta ya afya pekee, bali ni agenda ya maendeleo inayohitaji ushiriki wa sekta zote ili kujenga jamii yenye afya, nguvu kazi yenye tija na uchumi imara.



Amesema Mkoa wa Singida umeendelea kupata mafanikio katika kupunguza udumavu kwa watoto kutoka asilimia 29 hadi asilimia 25.7, lakini akasisitiza kuwa kiwango hicho bado ni kikubwa na kinahitaji hatua za haraka kupitia utekelezaji wa bajeti yenye matokeo. "Bila uwekezaji wa makusudi kwenye lishe, hatutafikia jamii yenye tija inayotarajiwa katika Dira ya Taifa ya Maendeleo," amesema.



Dkt. Mganga ameelekeza kuwa bajeti ya mwaka 2026/2027 izingatie utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Lishe kwa kuongeza fedha za ufuatiliaji wa watoto wenye utapiamlo, upatikanaji wa virutubisho, elimu ya lishe kwa jamii, huduma za lishe kwa mama na mtoto pamoja na kuimarisha huduma hizo katika ngazi ya kata na vijiji.



Aidha, amesisitiza kuwa kila sekta inapaswa kuwa na mchango unaopimika katika kuboresha hali ya lishe, huku akiitaka Serikali za Mitaa kutenga bajeti mahsusi kwa ajili ya kampeni za lishe shuleni, afya ya mama na mtoto pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta za afya, elimu na kilimo ili kuongeza upatikanaji wa chakula bora na salama.



Amesema Kamati ya Lishe ya Mkoa itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa viashiria vya lishe, huku akisisitiza kuwa taarifa za utekelezaji zinapaswa kuonesha matokeo halisi kwa wananchi badala ya kuishia kwenye takwimu pekee.



Wajumbe wa Kamati ya Lishe kwa upande wao wameeleza kuwa kuingizwa kwa afua za lishe katika bajeti ya mwaka 2026/2027 kutasaidia kupunguza mzigo wa magonjwa yanayotokana na utapiamlo, kuongeza tija ya nguvu kazi na kuharakisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii katika Mkoa wa Singida.



Kikao hicho kilihitimishwa kwa azimio la kuhakikisha bajeti ya mwaka wa fedha 2026/2027 inakuwa bajeti ya matokeo katika sekta ya lishe, kwa lengo la kuharakisha mapambano dhidi ya utapiamlo, kuboresha afya ya mama na mtoto na kujenga jamii yenye afya, uzalishaji na maendeleo endelevu.






















No comments:

Post a Comment