Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.Halima Dendego, ameitaka jamii pamoja na viongozi wa ngazi mbalimbali kuongeza juhudi katika kuhamasisha lishe bora kwa vijana ili kuimarisha afya na ustawi wa kizazi cha sasa na kijacho mkoani humo.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC) kilichofanyika Machi 8, 2026 katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Singida, Dendego alisema ni muhimu kwa wadau wote kushirikiana kuhakikisha vijana wanapata chakula cha kutosha na chenye virutubisho muhimu kwa maendeleo yao ya kimwili na kiakili.
Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi wa serikali pamoja na wataalamu wa afya ambao waliwasilisha taarifa kuhusu hali ya lishe kwa vijana mkoani humo.
Akiwasilisha taarifa hiyo, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Singida, Victorina Ludovick, alisema tathmini iliyofanyika inaonesha umuhimu wa kuendelea kuimarisha mikakati ya lishe bora kwa vijana wa umri wa miaka 15 hadi 19 ili kuwasaidia kufikia ukuaji wenye afya njema.
Alieleza kuwa juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha vijana wanapata chakula cha kutosha wakiwa shuleni na hata wanapokuwa nyumbani, hali itakayosaidia kuimarisha afya zao na uwezo wao wa kujifunza.
Akizungumzia suala hilo, Dendego alisisitiza umuhimu wa jamii kuendelea kuhamasishana kuhusu lishe bora ili kuhakikisha vijana wanapata chakula chenye virutubisho vinavyohitajika kwa maendeleo yao.
“Ni wajibu wetu sote kuendelea kuelimishana na kuhamasishana ili vijana wetu wapate lishe bora. Hii itasaidia kujenga kizazi chenye afya na nguvu ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia na taifa,” alisema Dendego.
Aliongeza kuwa lishe bora ina mchango mkubwa si tu katika ukuaji wa mwili bali pia katika afya ya muda mrefu na ustawi wa vijana wanapokuwa watu wazima.
Aidha, aliwataka wazazi na walezi kuwahamasisha vijana kula vyakula vyenye lishe bora na kupunguza utegemezi wa vyakula visivyo na virutubisho vya kutosha.
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Fatuma Mganga, aliwahimiza wazazi kuwafungashia watoto chakula wanapoenda shuleni ili kuwasaidia kupata lishe bora wakati wa masomo.
Alisema hatua hiyo itawasaidia wanafunzi kupata nishati na virutubisho vinavyohitajika ili kuendelea na masomo yao kwa ufanisi.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida (Ilongero), Eliya Dighah, alisisitiza umuhimu wa viongozi katika maeneo yao kuendelea kutoa elimu ya lishe kwa vijana ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi kuhusu vyakula wanavyotumia.
Katika kikao hicho pia ilisisitizwa kuendelea kuimarisha utekelezaji wa Mkataba wa Lishe katika ngazi ya halmashauri pamoja na kuhakikisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya lishe zinatumika ipasavyo ili kuimarisha afya ya wananchi, hususan vijana.


No comments:
Post a Comment