Wananchi zaidi ya 2687 wa mkoa wa Singida kutoka Halmashauri Saba za mkoa huo wamenufaika na upatikanaji huduma za matibabu ya kibingwa na bobezi kutoka kwa Madaktari bingwa 40 wa Rais Samia waliokuwepo katika mkoa wa Singida kwa muda wa siku Saba (7).
Kati ya idadi hiyo wananchi 69
wakiwemo watoto wamefanyiwa upasuaji kwenye Hospitali na Vituo vya Afya vya
mkoa wa Singida badala ya kupewa rufaa kwenda kwenye hospitali kubwa.
Akipokea Taarifa kwa niaba ya Mkuu
wa Mkoa wa Singida kutoka kwa Madaktari bingwa kuhusu namna zoezi la utoaji wa
matibabu lilivyofanyika, Katibu Tawala wa Mkoa Singida Dkt. Fatuma Mganga,
amewapongeza na kuwashukuru madaktari hao kwa kazi kubwa waliyoifanya kwa siku hizo
kwa kuwapatia wananchi matibabu ya kibingwa na bobezi karibu na maeneo yao.
Amesema ujio wa madaktari bingwa na
bobezi mkoani Singida pamoja na kutoa matibabu kwa wananchi wamesaidia kutoa
elimu kwa Watalaamu wa afya wa kada mbalimbali hali ambayo itasaidia kuimarisha
utoaji wa huduma za kiafya kwa wananchi wa mkoa wa Singida.
Kuhusu tatizo la upungufu wa
Watalaam katika sekta ya afya, Katibu Tawala huyo wa mkoa amesema Serikali ya mkoa
imejipanga vizuri ili kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi haraka ili
wananchi waweze kupata huduma zote muhimu kwenye Hospitali na Vituo vya afya
karibu na maeneo yao.
Nao baadhi ya Viongozi wa madaktari
bingwa na bobezi waliokuwa wanatoa matibabu kwa wananchi mkoani humo
wameipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuanzisha mkakati
maalum kwa Madaktari bingwa kwenda maeneo mbalimbali nchini ili kutoa matibabu
kwa wananchi ambao hawana uwezo wa kusafiri kwenda kwenye hospitali kubwa kwa
ajili ya kupata matibabu ya kiafya.
MATUKIO KATIKA PICHA WAKATI WA HAFLA YA KUWAAGA MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMI
No comments:
Post a Comment