Friday, September 16, 2022

MAAFISA AFYA SINGIDA WAAGIZWA KUWACHUKULIA HATUA BAADHI YA WATU WANAOCHAFUA MAZINGIRA

MAAFISA Afya mkoani Singida wameagizwa kuzitumia sheria zilizopo kwa kuwachukulia hatua baadhi ya watu wanaochafua mazingira maeneo mbalimbali ya mijini na vijijini yakiwamo ya barabara kuu na kwenye makaburi.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko, ametoa agizo hilo leo tarehe 16 Septemba, 2022 wakati wa kikao kazi cha Maafisa Afya kutoka halmashauri za mkoani hapa katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), Dk. Victorina Ludovick.

Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), Dk. Victorina Ludovick akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.

Alisema Serikali ya awamu ya sita inathamini sana suala la usafi wa mazingira kwani ndio mhimili mkubwa wa Afya ya Watanzania na ukuaji wa uchumi.

"Tumieni sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 na kanuni zake, sheria ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 pamoja na sheria ndogo za miji kuhakikisha maeneo ndani ya Mkoa wa Singida hayachafuliwi hovyo ikiwemo barabara kuu, stendi, masoko, mitaro, maeneo ya wazi, makazi na makaburi," alisema.

Mwaluko alisema maeneo ya masoko na biashara  wananchi waweke vyombo vya kuhifadhia taka vyenye ukubwa wa kutosha kulingana na uzalishaji wa taka kwa lengo la kupunguza taka kuzagaa ovyo mitaani.

Alisema yapo baadhi ya magari ya abiria yanasimama maporini na abiria kuchimba dawa (kujisaidia) vichakani jambo ambalo halikubariki hivyo Maafisa Afya wahakikishe wanachukua hatua.

Mwaluko alisema Maafisa Afya wa Mkoa wa Singida wanafanya kazi vizuri kutekeleza kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira lakini lazima kuhakikisha fedha inayotolewa na Serikali matokeo yake yanaonekana.

Aliongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri, Waganga Wakuu, Maafisa Afya na Watendaji wa vijiji na kata wasimamie ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo bora.

Alisema taarifa zilizopo hadi 31 Julai, 2022 kaya zenye vyoo katika Mkoa wa Singida ni asilimia 99.2 na zisizokuwa na vyoo ni asilimia 0.8, zenye vyoo bora ni asilimia 62.1 kutoka asilimia 27.6 mwaka 2015.

"Mimi kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, sitavumilia kuona magonjwa ya aibu kama vile kipindupindu yakitokea katika mkoa wangu hivyo mjipange katika hili," alisema Mwaluko.

Aidha, alisema Maafisa Afya watambue kuwa wao  kama wasimamizi na wafuatiliaji Wakuu wa shughuli za chanjo, ukaguzi wa dawa, ukaguzi wa vyakula na ukaguzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya mashuleni na taasisi zote waongeze bidii kusimamia hayo.

Afisa Afya Mkoa wa Singida, Mgeta Sebastian akizungumzia hali ya mazingira kwa mkoa huo.

Naye Afisa Afya Mkoa wa Singida, Mgeta Sebastian amesema kwamba wakati sasa umefika kwa Maafisa Afya kuhakikisha wanasimamia ili kuweka mazingira safi maeneo yote ya mkoa huo.

Sebastian amesisitiza kuwa katika suala la usimamizi wa afya atakuwa mkali na kwamba afisa afya asiyetekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa atachukuliwa hatua ikiwamo kumripo kwa wakuu wake.

MATUKIO KATIKA PICHA

Mratibu wa Huduma za Chanjo mkoa wa Singida, Habibu Said Mwinory akizungumza wakati wa kikao hicho.


No comments:

Post a Comment