Monday, September 19, 2022

SINGIDA YAFANYA VIZURI SENSA YA WATU NA MAKAZI, KAYA ZAHESABIWA KWA ASILIMIA 123

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo akiwasilisha taarifa ya tathimini ya Sensa ya Watu na Makazi kwa mkoa wa Singida kwa Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo Septemba 19, 2022

MKOA wa Singida umefanikiwa  kuhesabu kaya kwa kiwango cha asilimia 123 na idadi ya majengo kwa asilimia 121 katika zoezi la Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika Agosti 23, mwaka huu.

Mratibu wa Sensa ya Watu na Makazi Mkoa wa Singida, Naing'oya Kipuyo, ameyasema hayo leo Septemba 19, 2022 wakati akitoa taarifa ya zoezi hilo kwa Kamisaa wa Sensa nchini, Anne Makinda katika kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambacho kilihudhuriwa na wajumbe wa Kamati ya Sensa ya Mkoa.

Alisema Mkoa wa Singida uliweka makisio ya kuhesabu kaya 319,816 lakini hadi zoezi linakamilika kaya zilizohojiwa ni 394,171 sawa na asilimia 123.

Kipuyo amesema kwa upande wa majengo makisio yalikuwa kuhesabu majengo 390,064 lakini hadi mwisho wa zoezi la Sensa ya Watu na Makazi majengo 470,034 yalifanyiwa.

Naye Kamisaa wa Sensa, Anne Makinda, amesema mafanikio makubwa yamepatikana kutoka na ushirikiano uliokuwepo kwa makundi yote wakiwamo wanasiasa, viongozi wa dini ambapo hakuna aliyepinga zoezi la sensa.

Makinda amewashukru wananchi kwa uzalendo wa nchi yao na kwamba hili limedhihirisha kuwa kumbe tukipanga jambo kwa kuweka  uzalendo mbele  hakuna linaloweza kushindikana.

Kamisaa wa Sensa ya Watu na Makazi, Anne Makinda akizungumza wakati wa kikao cha tathimini ya zoezi la Sensa kwa mkoa wa Singida. (kulia) Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko, (kushoto) Mratibu wa Sensa Mkoa wa Singida Naing'oya Kipuyo.

"Hatukusikia lapushalapusha Singida isipokuwa mikoa michache ambayo kulikuwa na changamoto kulipa makalani, kimsingi tuseme uzalendo unaweza kuondoa kila kitu kinachoweza kuwa mgogoro kwetu," amesema Makinda.

Naye Katibu Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko,  alisema mkoa uliuchukulia kwa uzito mkubwa zoezi la Sensa kwa kuhakikisha zoezi linaeleweka kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka vijijini.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko akizungumza wakati wa kikao cha tathimini ya Sensa ya Watu na Makazi mkoani hapa.

Mwaluko amesema watu walishiriki kwa uaminifu kiasi kwamba hata maeneo ambayo tulijua hatuwezi kuyafikia lakini yalifikiwa kutokana na ushirikiano wa Kamati za Sensa za wilaya na ngazi ya mkoa.

No comments:

Post a Comment