Tuesday, September 20, 2022

MWALUKO AKUTANA NA MUFTI WA TANZANIA

 

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko (kulia) akikabidhi mchango wake kwa Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zuberi, kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Mufti Tanzania uliozinduliwa kitaifa Mkoani hapo Septemba 19, 2022.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko jana amekutana na Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zuberi ofisini kwake alipokuwa akitambulisha shughuli ya uzinduzi wa mfuko wa Maendeleo wa Mufti Tanzania uliozinduliwa kitaifa Mkoani hapo Septemba 19, 2022.

Akieleza umuhimu wa mfuko huo Sheikh Mkuu amesema mfuko huo utawasaidia wanafunzi zaidi ya 4000 nchini ambao wana mazingira magumu ya kupata elimu.

Aidha mfuko huo pia utaisidia jamii kwa kuwa unatumika kujenga mashule na hospitali katika maeneo mbalimbali hapa nchini pamoja na kutoa mikopo isiyokuwa na riba kwa wanawake.

Mufti ameeleza kwamba chanzo cha fedha za mfuko huo ni michango kutoka kwa watu mbalimbali hapa nchini wakiwemo jamii, Waislamu na wasiokuwa Waislaamu lengo likiwa ni kuondoa changamoto na fedheha zinazoikumba jamii ya Watanzania.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa wa Singida Dorothy Mwaluko akipokea ugeni huo amewahakikishia kupata ushirikiano mkubwa kwa Wana Singida wakati wa uzinduzi wa mfuko huo. 

Aidha, akipongeza Taaisisi hiyo ya BAKWATA kwa kuanzisha mfuko wa Maendeleo wa Mufti Tanzania unaolenga kuisaidia jamii ya watu mbalimbali Mwl. Mwaluko amechangia kiasi cha Tsh. Laki tatu (300,000) kwa ajili ya kutunisha mfuko huo.

Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Abubakar Zuberi, (kushoto) amshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Singida Mwl. Dorothy Mwaluko kwa mchango wake kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo wa Mufti Tanzania uliozinduliwa kitaifa Mkoani hapo Septemba 19, 2022.

No comments:

Post a Comment