Tuesday, September 24, 2024

RAS Singida Aagiza Usimamizi Bora wa Miradi ya Ujenzi 2024/2025

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amewataka Wakurugenzi, Maafisa manunuzi, na Wahandisi wa mkoa huo kuhakikisha kuwa miradi yote inayotekelezwa inakamilika kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa thamani sahihi ya fedha. 

Akizungumza kwenye kikao kazi na Watendaji wa Serikali kilichofanyi Septemba 24, 2024 katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo, Dkt. Mganga amesisitiza umuhimu wa kutoa huduma bora kwa wananchi kupitia usimamizi mzuri wa miradi ya serikali.

Dkt. Mganga amewasihi Wakurugenzi kuongeza umakini katika usimamizi wa rasilimali fedha za miradi inayotekelezwa katika halmashauri akisema Serikali inapoleta fedha inakuwa imeshafanya tathimini kwa kina kuhusu gharama za ukamilishaji wa miradi huku akiwasisitizia kuajili wakandarasi wenye uwezo na weledi ili kuepukana na makosa ya ujenzi na kuokoa muda wa ukamilishaji wa mradi.

Aidha, amewasisitiza Wahandisi wa halmashauri zote kusimamia kikamilifu mafundi wa ujenzi ili kuhakikisha miradi inajengwa kwa ubora na kukamilika kwa wakati. 

“Ni lazima kila mmoja afanye kazi yake kwa uzalendo na kujituma ili wananchi wapate huduma zinazostahili.” Dkt. Mganga

Pia, aliwataka maafisa manunuzi kufanya kazi kwa ufanisi na kufuatilia bei za soko kabla ya kuagiza vifaa vya ujenzi ili kuepuka gharama zisizo za lazima.

Hata hivyo amesisitiza kwamba maafisa manunuzi wanapaswa kupitisha malipo ya serikali kwa utaratibu sahihi, huku akionya kwamba hatua kali zitachukuliwa kwa wale watakaoshindwa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi. 

Akizungumzia makadirio ya vifaa, Dkt. Mganga amehimiza umuhimu wa kuhakiki wanafanya makadirio yanayotakiwa, badala ya kukadiria kwa wingi hadi vifaa kubaki hivyo amewataka kuwa na mipango sahihi ili kuhakikisha rasilimali za serikali zinatumika kwa ufanisi.

Akimalizia hotuba yake Katibu Tawala huyo wa mkoa amewataka Wakurugenzi kutowaachia walimu na wataalamu wa afya kusimamia miradi ya ujenzi ili kuepukana na uharibifu wa miradi ya ujenzi. 

No comments:

Post a Comment