Mkuu wa mkoa wa
Singida Mheshimiwa Halima Dendego amewataka Maafisa Ugani mkoani humo kuwa
wabunifu katika kuleta mabadiliko kwenye kilimo na utendaji mzuri wa
kazi ili kurahisisha ufikiwaji na upatikanaji wa huduma wenye tija kwa
wakulima.
Dendego
ameyasema hayo leo (Septemba 2, 2024) kwenye hafla ya ugawaji wa vishikwambi
206 kwa Maafisa Ugani wa Halmashauri za mkoani Singida iliyofanyika katika
ukumbi wa mikutano wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo.
Aidha, Mkuu
wa mkoa amesisitiza utunzaji mzuri wa vishikwambi hivyo ili kuzifanya kudumu
kwa muda mrefu na utendaji bora wa kazi huku akiwataka maafisa
ugani hao kuhakikisha wanaishi karibu na maeneo yao ya kazi katika
kata na vijiji ili kurahisisha ufikiwaji na upatikanaji wao kwa wakati na
wananchi wanaohitaji huduma hizo.
Hata hivyo,
amewasisitiza uvaaji wa sare za kazi muda wote wawapo kazini ili kutambulika
kwa urahisi na wananchi wanaowahudumia katika kata na vijiji vyao na matumizi
sahihi ya vifaa walivyopewa ikiwemo vishikwambi, pikipiki na vipimia
udongo kama namna ya kuinua kilimo.
"Huwezi
kuwekeza kwenye kilimo bila kuwekeza kwenye wataalam, tunataka
mkaibadilishe Singida ili wanasingida warudi kwenye kilimo, hakuna
namna nyingine ya kumaliza hali duni Singida bila kujituma katika
kilimo". alisema RC. Dendego.
Pia, alihimiza
maafisa ugani kuhakikisha wanatumia vishikwambi kwa ajili ya kazi pekee na sio
shughuli binafsi, akibainisha kuwa vifaa hivyo vimetolewa na serikali ili
kuboresha huduma za kilimo na kuinua uchumi wa wakulima. "Ni lazima
tuhakikishe tunavitumia kwa lengo lililokusudiwa na kuleta matokeo chanya kwa
wakulima na jamii ya Singida kwa ujumla," alisema RC. Dendego.
Naye, Katibu
Tawala wa Mkoa wa Singida, Dk. Fatuma Mganga, ametoa rai kwa Maafisa ugani wa
mkoa huo kutumia vishikwambi walivyokabidhiwa na serikali kwa lengo la
kuboresha shughuli za uzalishaji, hususan katika sekta ya kilimo.
Dk. Mganga
alisisitiza kuwa vifaa hivyo ni muhimu katika kurahisisha ukusanyaji wa takwimu
na ufuatiliaji wa shughuli za kilimo kwa wakulima ili kuongeza tija na ufanisi.
Ameeleza kuwa
matumizi sahihi ya vishikwambi hivyo yatawawezesha maafisa ugani kuwa karibu
zaidi na wakulima, kutoa elimu ya kilimo, na kutambua changamoto wanazokutana
nazo kwa wakati.
Kwa upande wake Afisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida Natalya Mosha, ameishukuru serikali na kuahidi kuwafikia wakulima wengi kwa muda mfupi baada ya kupata vitendea kazi kama vishikwambi na pikipiki, kutoa maelekezo ambayo wananchi walikua hawawezi kuyapata na wakulima kuongeza uzalishaji katika maeneo yao na hatimaye kuongeza tija katika kilimo.
No comments:
Post a Comment