Friday, August 30, 2024

*RC DENDEGO AAHIDI KUUFANYA MKOA WA SINGIDA KUWA MIONGONI MWA MIKOA MITATU BORA KIUCHUMI*


Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, amesema dhamira yake ni kuhakikisha mkoa unaingia katika mikoa mitatu bora yenye uchumi wa uhakika.

Akizungumza  (28 Agosti, 2024) wakati wa kufungua kikao kazi cha siku tatu kinachowahusisha viongozi wa mkoa, wilaya, na tarafa, pamoja na sekta binafsi, kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa ofisi ya mkuu wa mkoa huo Dendego ameeleza kuwa matarajio yake ni kuona viongozi hao wanatoa mchango utakaosababisha mabadiliko chanya katika mkoa wa Singida.

Aidha, RC. Dendego amesema kikao hicho kinahusu kubadilishana uzoefu na kuweka malengo makubwa yanayopaswa kufikiwa na mkoa wa Singida, huku akisisitiza kuwa ni fursa ya kuamsha ari ya kutenda kazi kwa bidii ili kuwahudumia wananchi wa Singida ipasavyo.

Katibu Tawala Mkoa wa Singida,Dkt. Fatuma Mganga akiwasilisha mada katika mafunzo ya kujengeana uwezo viongozi wa serikali na sekta binafsi.

Pia, ameeleza kuwa kila mmoja anatambua mwelekeo wa nchi, hususan dhamira ya dhati aliyo nayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maendeleo ya Watanzania.

 RC Dendego amefafanua kuwa Rais Samia ameelekeza namna ya kufanya kazi kwa kuzingatia falsafa yake ya "R4," inayolenga kuhakikisha kila Mtanzania anafaidika na uwepo wao ndani ya taifa. Hivyo Dendengo amehimiza viongozi kushikamana na kujituma ili kuhakikisha Singida inafikia mafanikio makubwa katika nyanja mbalimbali za maendeleo ikiwa ni kuunga mkono juhudi hizo za Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Sehemu ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama Mkoa wa Singida wakiendelea na mafunzo.

Baadhi ya Viongozi wa Serikali na sekta binafsi Mkoa wa Singida wakiendelea na mafunzo.




No comments:

Post a Comment