Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe.
Halima
Dendego, amewataka viongozi wa mkoa huo kusimamia kikamilifu vyanzo vyote vya
mapato na kuhakikisha taratibu zote zinafuatwa kwa usahihi.
Akizungumza (Agosti 29,
2024) ikiwa ni siku ya pili katika kikao kazi na watendaji wa Serikali
pamoja na Sekta binafsi, Dendego amesisitiza umuhimu wa kuwa na nidhamu
ya mapato na uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya rasilimali za umma.
Amesema viongozi wanapaswa
kuhakikisha vyanzo vya mapato vinatambuliwa, kusimamiwa, na kudhibitiwa ili
kuzuia mianya ya upotevu wa fedha za umma. Ameongeza kuwa ukusanyaji wa
mapato lazima uendane na sheria taratibu na kanuni zilizopo ili kuimarisha
uwazi na uwajibikaji katika matumizi ya fedha.
“Kila kiongozi anawajibika
kuhakikisha mapato yanakusanywa ipasavyo na hakuna upotevu wa aina yoyote. Ni
jukumu letu kuhakikisha tunasimamia rasilimali hizi kwa uadilifu na kufuata
taratibu zote za kisheria,” alisema RC Dendego.
Aidha, ameonya dhidi ya vitendo vya
rushwa na matumizi mabaya ya ofisi, akisema ni jukumu la viongozi wote kuwa
mfano bora kwa kufuata sheria na taratibu katika utendaji kazi. Amesisitiza kuwa uwazi na
uwajibikaji ni msingi wa mafanikio ya mkoa na kwamba hakuna kiongozi anayepaswa
kukiuka taratibu za ukusanyaji na matumizi ya mapato.
Dendego pia amewataka viongozi kuwa
wabunifu na kutafuta vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza mapato ya mkoa
na taifa kwa ujumla, akisisitiza kuwa usimamizi mzuri wa vyanzo vya mapato utasaidia katika
utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maisha ya wananchi wa
Singida.
Amemalizia kwa kuwataka
viongozi wote kuhakikisha wanatekeleza wajibu wao kwa uadilifu na kuhakikisha
mapato yote yanakusanywa na kupelekwa benki kwa wakati huku akisisitiza umuhimu
wa kufuata taratibu zote zilizopo bila kuzipindisha.
Viongozi wa serikali na sekta binafsi wakiendelea na mafunzo.
No comments:
Post a Comment