Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, amewasihi wakazi wa mkoani humo kuweka nguvu kubwa katika kujikinga na ugonjwa hatari wa homa ya Nyani (M-Pox) unaosababishwa na virusi.
Dendego amebainisha kuwa ugonjwa huo hauna tiba ya moja kwa moja na bado haujasambaa wala kuingia nchini Tanzania, hivyo jitihada kubwa zinapaswa kuelekezwa katika kujiepusha na maambukizi yake.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akizungumza na wadau wa afya.Akizungumza leo (Septemba 3, 2024) katika mkutano wa wadau wa afya mkoani Singida uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mkoa wa huo, Dendego alihimiza jamii kuchukua tahadhari kwa kufuata njia mbalimbali za kujikinga ikiwemo kutumia vitakasa mikono.
Mkuu huyo wa mkoa ameweka wazi mikakati mbalimbali ya kuuweka Mkoa wa Singida salama dhidi ya ugonjwa wa M-Pox, ikiwa ni pamoja na kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja kupitia utoaji wa elimu kwa umma.
Alieleza kuwa njia kama vipindi vya redio na televisheni, pamoja na mafunzo ya moja kwa moja katika maeneo ya makazi na biashara, ni muhimu katika kuhakikisha ujumbe unawafikia watu wengi kwa wakati mmoja.
"Tuwekeze nguvu kubwa katika kujikinga na ugonjwa huu, tuwafikie watu wengi kwa wakati mmoja kwa kutumia redio na mafunzo juu ya ugonjwa huu yatolewe katika Shule, masoko, standi, maeneo ya kuabudu, pamoja na mikosanyiko," alisema Dendego.
Alisema kuwa mafunzo haya yanapaswa kuwa ya kina na kueleweka ili jamii iweze kuchukua hatua stahiki za kujikinga na kuzuia maambukizi mapya.
Aidha,
alieleza kuwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya habari utasaidia kuongeza
uelewa na kutoa taarifa sahihi kwa wananchi kuhusu ugonjwa huo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Mkoa wa Singida Martha Mlata (kushoto) akiwa na Katibu wa Chama hicho Lucy Boniface wakionesha mfano wa moja ya zoezi la utumiaji wa vitakasa mikono ikiwa ni sehemu ya kujikinga na maambukizi ya ugonjwa wa homa ya nyani (M-POX) mara baada ya kumaliza kikao.
No comments:
Post a Comment