Wednesday, June 21, 2023

Viwanja vilivyouzwa kwa mkopo Wilayani Manyoni kurudishwa Serikalini.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni kurejesha viwanja vyenye thamani ya Tsh. Milioni 533 ambavyo viliuzwa kwa mkopo ambapo vimesabasha hoja ya Ukaguzi.

Akiongea katika Kikao Maalum cha kupitia hoja za ukaguzi kilichofanyika leo tarehe 21.06.2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo alibainisha kwamba ili hoja hiyo ifungwe ni lazima kutolewa tangazo (notice) la kurejesha viwanja hivyo.

RC Serukamba amesema anatoa kipindi cha siku 7 (wiki moja)  Halmashauri hiyo iwe imetangaza kwenye vyombo mbalimbali vya habari ambapo tangazo hilo litatumika kama kiambatanisho cha kufunga hoja hiyo kwa kuwa viwanja vitakuwa katika umiliki wa Halmashauri hiyo.

Hata hivyo Serukamba ametoa onyo kali kwa watumishi na viongozi wa Halmashauri kuacha kuuza mali za umma kwa mkopo jambo ambalo amelieleza kwamba kuna uwezekano viwanja hivyo vimehodhiwa na watumishi hao.

"Iwe mwanzo na mwisho kuuza mali za umma kwa mkopo, na inawezekana viwanja hivyo vinamilikiwa na watumishi kama madalai ili wakiuza kwa faida ndio walipe madeni yao"  Serukamba.

Aidha Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Jumanne Mlagaza, amemueleza RC Serukamba kwamba baadhi ya Madiwani ni miongoni mwa ambao waliochukua sehemu ya viwanja hivyo na kutovilipia hivyo kuwataka kuvilipia kabla ya matangazo ama sivyo kuvirejesha Halmashauri.

Kwa upande wake Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga, amekemea tabia ya kutokamilisha miradi kwa vigezo vya kwamba fedha hazitoshi wakati kila ujenzi Serikali ilishafanya hesabu na kubaini fedha wanazozituma.

Ras ameeleza kwamba miradi mingi haikamiliki kwa sababu Maafisa ugavi kuongeza fedha jambo ambalo husababisha kutumia fedha nje ya bajeti na kusababisha hoja za ukaguzi.

Amewaomba Madiwani kuwa sehemu ya miradi ili kusaidia uhamasishaji kwa wananchi kushiriki nguvu kazi ili kupunguza gharama za ujenzi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba, akisisitiza jambo wakati wa Kikao Maalum cha kupitia hoja za ukaguzi kilichofanyika leo tarehe 21.06.2023 katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Jumanne Mlagaza, akizungumza wakati wa kikao hicho.

Sehemu ya Wajumbe kutoka Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mkoa wa Singida wakiwa katika kikao hicho.








No comments:

Post a Comment