Wednesday, June 21, 2023

Serukamba awataka wenye Malori kupaki ndani ya Kituo cha mabasi cha Manyoni.

Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Mkoani Singida leo tarehe 21.06.2023 wametakiwa kutumia Kituo cha mabasi makubwa na madogo cha mjini hapo kuegesha malori muda wa usiku wakati mchana wakiendelea na huduma za mabasi hayo.

Maagizo hayo yametolewa na Mkuu wa Mkoa huo Peter Serukamba, wakati wa Baraza la Madiwani lililokutana kupitia hoja za ukaguzi ambapo alibainisha kwamba ili kuongeza mapato ya Halmashauri hiyo lazima chanzo hicho kitumike kupata fedha.

Amesema mwezi kuanzia tarehe 1 hadi tarehe 31 mwezi wa tano wakati malori yakipaki nje ya kituo cha mabasi walikusanya jumla ya Tsh.Milioni 2 na laki moja (2,100,00) lakini baada ya malori kuamriwa kupaki ndani ya Kituo cha mabasi kwa siku nane  (8)  walikusanya zaidi ya  Tsh.Milioni 1 na laki Tano (1,500,000).

RC amewataka Madiwani wa Halmashauri hiyo kuunga mkono kwa sababu fedha zitakazopatikana ni kwa ajili ya maendeleo ya Halmashauri ya maendeleo kwa wananchi wa Manyoni.

Hata hivyo amesisitiza kwamba zoezi la makusanyo ya mapato ni suala la kufa na kupona hivyo hategemei kuona watu wakienda kinyume na makubaliano hayo.

Kwa upande wake Dkt. Pius Chaya Mbunge wa Manyoni  amesema wao walijaribu kuweka askari kwenye geti la Kintinku ambapo mapato yaliongezeka kutoka Milioni 2.5 kwa mwezi hadi kufikia zaidi ya Milioni 20 kwa mwezi hivyo akimhakikishia RC kwamba watamuunga mkono kufanikisha hilo.

Akikomelea hoja ya kuinua mapato Wilayani Manyoni Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga ameshauri kuboreshwa vibanda  vilivyopo ndani ya stendi hiyo ili iwe ni chanzo cha uhakika ili kubadilisha hali ya makusanyo eneo hilo.



Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba akizungumza wakati wa kikao hicho.


Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni Jumanne Mlagaza, akizungumza wakati wa kikao hicho.


Sehemu ya Meza Kuu.

No comments:

Post a Comment