Friday, June 23, 2023

Singida waamua kutumia CcTv Kamera kuondoa ukatili wa watoto shuleni

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amesema matumizi ya teknolojia ya kamera za usalama (CCTv Camera) itumike kukomesha ukatili dhidi ya watoto hasa shuleni.

RAS amesema hayo leo (Juni 23, 2023) alipokutana na wadau wa elimu katika ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa huo ambao umelenga kuweka mkakati wa Mkoa wa kuwalinda watoto wa shule dhidi ya vitendo vya ukatili.

Amesema kamera zikiwepo katika korido ya vyoo vya shule, madarasani na kwenye magari ya kusafirishia watoto zitasaidia kuwatia hofu wenye nia ovu dhidi ya watoto na zitasaidia kupata ushahidi pindi watoto wanapofanyiwa ukatili.

Pamoja na hayo Katibu Tawala ameagiza maafisa elimu kuhakikisha vipindi vya dini shuleni vinatekelezwa kwa ufasa na watoto kuhudhuria kikamifu na usiwe kwamba ni kwa mwanafunzi anayetaka, huku akiwataka viongozi wa dini kuhakikisha kwamba wanakemea vitendo hivyo vya ukatili dhidi ya watoto.

Aidha RAS amebainisha kwamba utafiti ulifanyika mwaka 2015/16 ( Tanzania Demographic and health Survey) zinaonesha kwamba 40% ya wanawake katika umri wa miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa vitendo vya ukatili, na 10% ya wanawake wenye umri huo wamefanyiwa ukeketaji.

Hata hivyo ameeleza kwamba  utafiti mwingine uliofanyika mwaka 2009 (The Survey on violence  against children) unaonesha kwamba asilimia 28 ya wasichana na asilimia 13 ya wavulana wamefanyiwa ukatili wa kingono ambayo yametokewa maeneo ya nyumbani.

RAS Mganga ameendelea kueleza kwamba asilimia 73 ya wasichana na 72 ya wavulana wamefanyiwa ukatili wa kimwili kati yao asilimia 60 hufanyiwa na ndugu zao.

Akimalizia hotuba yake amewaagiza maafisa elimu wote kuhakikisha shule zote zinakuwa na madawati ya ulinzi na usalama shuleni ili watoto waweze kujadili masuala ya ukatili.

Awali akifungua kikao kazi hicho Mganga Mkuu wa Mkoa Victorina Ludovick, alisema kikao kina lenga kuwajengea uwezo washiriki na wadau wote kutumia mbinu rafiki ya uelimishaji ili waweze kupaza sauti zao kuzuia ukatili dhidi yao.

Mganga Mkuu wa Mkoa Victorina Ludovick, akizungumza wakati wa kikao hicho.







Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga akisisitiza jambo wakati wa kikao hicho.

No comments:

Post a Comment