Wednesday, February 01, 2023

Mahakimu Mkoani Singida wakumbushwa kuwatendea haki Wananchi.

 

Mahakimu na Wasimamizi wa Sheria Mkoani Singida wametakiwa kuepuka vitendo vya kupokea rushwa ambayo unaosababishwa upindishwaji wa Sheria ili kuwatendea haki wananchi huku wakihimizwa  kusaidia kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi.

Maelezo hayo yametolea leo na Jaji Mstaafu Fatuma Massengi wakati wa kilele cha wiki wa Sheria inayoadhimishwa kila tarehe 1 Februari Nchini, maadhimisho ambayo Mkoa wa Singida zimeadhimishwa katika viwanja vya Mahakama ya Mkoa iliyopo mjini Singida.

Jaji Massengi amesema katika vitabu vya dini vimeeleza kwamba Mahakimu watakuwa wa mwisho kuingia mbinguni kwa kuwa maswali yatakuwa mengi hasa kwa wale ambao hawakuwatendea haki wanaanchi.

Aidha amewaasa Mahakimu kutenda haki na kusimamia Sheria kwa kuwa kazi hiyo ni kazi ya Mungu na ni msingi wa Maendeleo ya nchi ambapo kama Sheria itapindishwa itasababisha kudumaza uchumi wa nchi.

"Tuache kupokea rushwa kwa kuwa inadidimiza uchumi, napenda kuwakumbusha Mahakimu kuhakikisha wanatenda kazi ya Mungu bila upendeleo, vitabu vya dini vinaeleza kwamba Mahakimu watakuwa wa mwisho kuingia mbinguni kwa kuwa watakuwa na maswali mengi ya kujibu" Alisema Jaji Fatuma.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amewaomba wanasheria wa Serikali na Binafsi kuambatana naye kila wiki ya tatu ya kila mwezi kwenda Wilayani kutatua kero za Wananchi badala ya kusubiri maofisini.

Aidha amewataka Maafisa wa Mahakama kuongeza jitihada ya kutoa elimu kwa wananchi ambao hawajui umuhimu wa kutatua migogoro yao nje ya Mahakama ili kuwapunguzia gharama kupeleka mashtaka Mahakamani ambayo yangeweza kutafutiwa kwa usuluhishi.

"Tumeanzisha utaratibu wa kuwafuata wananchi walipo kwenda kusikiza changamoto zinazowakabili hivyo niwaombe mawakili wa Serikali na Binafsi tuwe tunaambatana kwenda kutatua migogoro kwa njia ya usuluhishi walipo wananchi". Serukamba

Hata hivyo amepongeza Mahakama kwa kuwa mabingwa wa kutumia teknolojia ya Habari kutatua kuendesha mashtaka na kupunguza mrundikano wa kesi katika Mahakama zao.

Naye Hakimu mkazi wa Mahakama kuu ya Singida Allu Nzowa amesema Mahakama imejipanga kuhakisha kwamba katika mwaka mpya wa Sheria watahakikisha haki za watu zinapatikana kwa wakati.

Nzowa amewataka wananchi kuepuka migogoro kwa sababu imekuwa chanzo cha kudidimiza uchumi kwa wananchi na kuleta umaskini kwakuwa watu wanashindwa kuendelea kuzalisha au kufanya biashara kwa sababu ya migogoro.

Awali Mkuu wa Mashtaka Mkoa wa Singida  Juma Hasani Salige alieleza kwamba wananchi wanapata changamoto kuendesha migogoro kwa gharama kubwa huku ikisababisha kupungua na kudhoofika kwa uchumi wao, huku mwakilishi wa Chama cha Mawakili wa kujitegemea (LLS) Salma Musa,  aliomba wanasheria binafsi washirikishwe kwenye utatuzi wa migogoro kwa njia ya usuluhishi na kupatiwa jengo la ofisi Mkoani hapa.

MATUKIO MBALIMBALI KATIKA PICHA













No comments:

Post a Comment