Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, ameagiza
kukamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria kwa wanafunzi wa kike waliopata
mimba wakiwa shuleni wakiwemo wazazi kama hatua ya kukomesha tatizo hilo ambayo
limeonekana kuwa ni kero kubwa katika maendeleo ya sekta elimu mkoani humo.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti katika
ziara yake ya kikazi ya Siku Mbili katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi wakati
anakagua ujenzi wa miradi ya maendeleo pamoja na kuzugumza na wananchi katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Kijiji Songambele mjini
Itigi ili kutatua kero zinazowakabili.
Dendego, amesema ili kukomesha tatizo hilo yeye ataanza
kukamata kwanza msichana aliyepata mimba na baadaye mvulana ambaye atakuwa mtuhumiwa
namba mbili kama hatua ya kukomesha vitendo vya mimba kwa wanafunzi.
“Nikikuta msichana umepata mimba wewe utakuwa mshtakiwa namba Moja na
wewe ndio utakayeenda jela bila huruma na tumbo lako utajifungulia huko huko
kwa sababu mna tabia ya ukipata mimba tunaenda kukimbizana na mtoto wa kiume si
sawa wote mlishirikiana kwa hiyo yeye atakuwa mstakiwa namba mbili na msichana
atakuwa mstakiwa namba Moja,” Amesisitiza RC Halima Dendego.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego (wa kati waliokaa) akizungumza na Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Kitaraka iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Itigi mara baada ya kukagua ujenzi wa nyumba za Walimu.
Kuhusu wanafunzi 4,000 kutoripoti shuleni mkoani Singida
hadi sasa, Mkuu wa mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego, ametoa muda wa mwezi
Mmoja kwa Makatibu Tarafa na Maafisa Watendaji wa Vijiji na Kata wahakikishe
wanawasaka wanafunzi hao popote walipo na kuwarudisha shuleni vinginevyo
watakiona cha moto.
Amesema itakuwa jambo la aibu kwa Serikali kujenga shule kwa
gharama kubwa huku wanafunzi wanaotakiwa kusoma kwenye shule hizo hawapo
shuleni na kusisitiza kuwa hatakubali hata kidogo aibu hiyo imkute na ni lazima
wanafunzi hao wasakwe popote walipo ili warudishwe shuleni wakasome.
RC Dengedo, ameagiza kupatiwa taarifa zote za wanafunzi wa
shule za Msingi na Sekondari ambao hawajaripoti shuleni mpaka sasa hata kama
wamehama na shule walipohamia ili aweze kufuatilia kama ni kweli yupo kwenye
shule hiyo au ni uongo.
Naye, Katibu Tawala wa mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa mfano kwa wazazi na jamii nzima na kuachana na mambo yanaenda kinyume cha maadili ya Kitanzania.
Dkt. Fatuma Mganga, amesema kuwa kama wanafunzi watasoma kwa
bidii hadi Vyuo Vikuu watakuwa na faida kubwa sio tu kwa familia zao bali kwa
jamii nzima na Taifa kwa ujumla kwa sababu Serikali imeboresha mazingira ya
kujifunzia na kufundishia.
No comments:
Post a Comment