Monday, April 15, 2024

RC DENDEGO ATOA WITO KWA WAZAZI KUPELEKA WATOTO WA KIKE KUPATA CHANJO YA SARATANI

MKUU wa Mkoa wa Singida, Halima Dendego, amewataka viongozi mbalimbali wakiwamo viongozi wa Dini kuwaelimisha Wazazi wenye watoto wa kike wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 kuwapeleka kupata chanjo ya Saratani ya Mlango wa kizazi itakayoanza kutolewa mkoani hapa April 22, 2024.

Alitoa agizo hilo (Aprili 15, 2024) wakati wa kikao cha uhabarisho ngazi ya Mkoa kilichowajumuisha Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Dini, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wataalamu wa afya kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Singida.

Amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na mwana Mama Shupavu Dkt. Samia Suluhu Hassan imeweka mikakati ya kuhakikisha wanawake wanapewa chanjo wenye umri kati ya miaka 9 hadi 14 lengo kuwafanya wanapofikia umri wa kuwa 'active' katika masuala ya kujamiana wawe na kinga hasa kutokana ugonjwa huu unaambukiza kirahisi kwa njia ya kujamiana.

"Leo tumeitana kama wajumbe wa kamati na kama viongozi kwneye jamii tunajua jamii zetu zina mitazamo tofauti na tunaishi kwenye mila na desturi tofauti lakini hili lazima tuungane sote kwasababu madhara ya ugonjwa huu yanatuathiri sisi wote bila kuangalia tofauti ambazo tunazo," amesema Dendego.

Dendego amesema ili kuweza kufanikisha chanjo hii viongozi wote ambao wana ushawishi mkubwa kwenye jamii wasaidie kuwahamisha wazazi ambao wana wasichana wenye umri wa kuanzia miaka 9 hadi 14 kuhakikisha wanapata chanjo ya saratani ya mlango wa uzazi.

"Chanjo hii inatolewa bure, sote tunatambua mwanamke ndo mlezi wa familia na mwanamke pia ana mchango mkubwa katika maendeleo ya uchumi,kwa hiyo muda wote tunataka wamama wawe salama ili watimize jukumu lao la kibailojia walilopewa na mwenyezi Mungu lakini pia watimize majukuya kijamii na kiuchumi," amesema Dendego na kuongeza kuwa.....

"kwa hiyo niwaombe sana tutumie foramu na majukwaa tuliyonayo tuweze kutangaza ili chanjo na habari hizi ziweze kuwafikia wananchi wengi wa Singida,"

Naye Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginoma, amesema walengwa wa chanjo ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa mwaka 2024 ni wasichana wote wenye umri wa miaka 9 hadi 14 waliozaliwa kati ya 2010 hadi 2015.

Amesema zoezi hilo litaanza rasmi Aprili 22 hadi 26 mwaka huu na kuendelea hadi Disemba ili kuwafikia walengwa wote ambapo kwa Mkoa wa Singida   wasichana 178,114 wanatarajia kupewa chanjo hiyo ambapo tayari dozi 191,040 zimeshapokelewa na usambazaji kwenye ngazi ya halmashauri unaendelea.

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, akizungumza kwenye kikao hicho na Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Viongozi wa Dini, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na wataalamu wa afya kutoka Wilaya zote za Mkoa wa Singida.

Mratibu wa Huduma za Chanjo Mkoa wa Singida, Jadili Mhanginoma, akitoa taarifa ya utoaji wa chanjo ya HPV dhidi ya Saratani ya mlango wa kizazi kwa wasichana wenye umri wa miaka 9 hadi 14, kwenye kikao hicho.

Kikao kikiendelea.

No comments:

Post a Comment