Wednesday, April 24, 2024

RC DENDEGO: SEKTA YA BIASHARA NA VIWANDA NI MUHIMU KWA UCHUMI WA MKOA WA SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mheshimiwa Halima Dendego, amekutana na Uongozi wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) wa mkoani humo, leo Aprili 24, 2024 ofisini kwake, na kufanya nao mazungumzo yanayohusiana na sekta ya biashara ili kukuza na kuinua uchumi wa mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kupitia kikao hicho, ujumbe wa TCCIA Mkoa wa Singida uliyoongozwa na Mwenyekiti wake Bw. Elly Kitila Mkumbo, ukiwa na lengo kwa Jumuiya hiyo ya Wafanyabiashara kujitambulisha mbele ya Mkuu huyo wa Mkoa aliyehamia Singida kutokea Mkoani Iringa hivi karibuni.

Aidha, katika kikao hicho walipata wasaa wa kujadili fursa mbalimbali kupitia Sekta ya biashara, uchumi, uzalishaji pamoja na uwekezaji zilizopo mkoani Singida hususani kwenye viwanda, kilimo, biashara, uvuvi, mifugo, madini, pamoja na miundombinu ya barabara na nishati ili ziweze kuinua na kuboresha maisha wananchi wa mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

RC Dendego, ameuhakimishia uongozi wa Jumuiya ya Wafanyabishara hao kuwa ataimarisha ushirikiano zaidi baina ya pande zote mbili ili kukuzu uchumi wa wanasingida kupitia sekta binafsi kwakuwa Serikali ya Mkoa ipo imara katika Ulinzi na Usalama.

“Kwa kweli Jumuiya yenu ya Chamber of Commerce, ni muhimu na ni muhimili mkubwa katika uchumi, niwaombe sana tuendeleze ushirikiano huu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu ambao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja ndio maana miradi mbalimbali inatekelezwa.’ amesema Dendego.

Katika mazungumzo hayo, msafara wa Jumuiya ya Chamber of Commerce, kupitia Mwenyekiti Kitila, alimweleza Dendego umuhimu wa Serikali kuboresha soko la kimataifa la vitunguu lililopo Kata ya Misuna katika Manispaa ya Singida kutokana na umuhimu wake katika kuhudumia wakulima na wafanyabishara wa ndani na nje ya Tanzania. 

Kitila amemhakikishia Mkuu huyo wa mkoa kuwa, Chamber of Commerce itaendeleza na kudumisha ushirikiano baina ya Jumuiya ya TCCIA na Serikali kwa nia thabiti ya kumkomboa na kuhakikishia mfanyabiashara shughuli zake zinatekelezeka kwa maslahi ya Taifa pamoja na kulitangaza soko la kimataifa la vitunguu lililopo mkoani Singida.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wakulima na wenye Viwanda Tanzania (TCCIA) Mkoa wa Singida Bw. Elly Kitila Mkumbo, akizungumza kwenye kikao baina ya Mkuu wa Mkoa wa Singida na TCCIA kilichofanyika ofisini kwa Mkuu wa Mkoa huo.

Kuhusu sekta ya Mawasiliano, mmoja wa wajumbe wa Chamber of Commerce, James Japheth (Buhanzo), ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Standard iliyopo Singida Mjini ameahidi kuongeza wigo wa usikivu wa Redio hiyo aliyowekeza mkoani humo ili masafa yake yaweze kupatikana kwa urahisi ndani na nje ya mkoa wa Singida.

Buhanzo alilazimika kusema hayo, baada ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, kumtaka atumie fursa ya uwekezaji wa kituo chake cha Redio kuongeza usikivu wa matangazo ili Wananchi wa mkoani humo waweze kupata habari mbalimbali za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali pamoja na sekta binafsi.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, akisisitiza jambo kwa Wajumbe wa kikao hicho.


Kikao kikiendelea.

No comments:

Post a Comment