Tuesday, April 23, 2024

KUELEKEA MAADHIMISHO YA MIAKA 60 YA MUUNGANO, RC SINGIDA AHIMIZA AMANI NA UTULIVU

Mkuu wa mkoa wa Singida Halima Dendego ameonya kuwa atawachukulia hatua kali watu au kikundi cha watu wanaotaka kuvuruga au kuvunja amani na utulivu kwa wananchi wa mkoa wa Singida.

Dendego, ametoa kauli hiyo (leo 23/Aprili/24 ) mjini Singida, katika uzinduzi wa wiki ya maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa kufanya usafi katika maeneo mbalimbali ya Soko Kuu la Singida.

Mkuu huyo wa mkoa wa Singida amewasisitiza wananchi wa mkoa wa Singida kuwakataa watu au mtu yeyote anayetaka kumdhalilisha Rais au Watanzania kwani wakiwaruhusu kufanya hivyo watakuwa wamedhalilisha Taifa na Watanzania wote hivyo ni lazima wananchi wote waungane kukataa watu hao wenye nia mbaya na Taifa la Tanzania.

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego, (wapili kushoto) akifanya usafi wa mazingira na wananchi katika soko kuu la Singida.

“Tuungane wote katika kupambana na yeyote anayetaka kuleta ujinga ujinga katika Taifa letu tuwabaini ili tuwawajibishe “ Amesisitiza Halima Dendego.

RC Dendego, amesema yeye ni rafiki wa wote Vijana, Wazee, Wanaume na Wanawake hivyo Ofisi yake ipo wazi muda wote kwa anayetaka kusaidiwa kwa shida yeyote aende ili asaidiwe nia ni kuona wananchi Singida wanaishi maisha mazuri na yenye staha bila kero.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhe. Godwin Gondwe amemhakikishia Mkuu wa mkoa huo kuwa atasimamia maelekezo yake yote aliyotoa hasa ya kuhakikisha Manispaa ya Singida inakuwa safi katika maeneo yote ya Masoko na maeneo yenye watu wengi kama hatua ya kudhibiti magonjwa ya maambukizi ikiwemo kipindupindu.

Gondwe amesema kuwa hivi karibuni watazindua kampeni kubwa ya usafi katika Manispaa ya Singida ambayo itasaidia kuboresha usafi katika maeneo yote ya mji wa Singida ikilinganishwa na hali ilivyo sasa.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Singida, Edward Mboya amebainisha kuwa kupitia mapato ya ndani wanaendelea na mchakato wa kununua gari nyingine mpya ya kubebea taka na vifaa vya kuhifadhi taka lengo likiwa ni kuifanya Manispaa ya Singida kuwa bora nchini hasa katika masuala ya Usafi.

Mkuu wa Wilaya ya Singida Godwin Gondwe, akifanya usafi wa mazingira na wananchi katika soko kuu la Singida.

Wananchi wa Singida Mjini wakifanya usafi wa mazingira ikiwa ni sehemu ya kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment