Monday, November 28, 2022

Ofisi za Shule Bora zafunguliwa rasmi Mkoani Singida.

 

Mkoa wa Singida umesema mikakati mbalimbali ya kuboresha ufundishaji na ujifunzaji wa elimu katika shule za Sekondari na Msingi kama sehemu ya ushirikiano na wadau wengine wakiwemo shule bora katika kuimarisha elimu kwa watoto wote.

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Stanslaus Choaji, wakati wa uzinduzi wa Ofisi ya Mradi wa shule bora Mkoa wa Singida ambapo alieleza juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau hao kuboresha ujifunzaji, ufundishaji na ujumuishi wa elimu ya Msingi na Sekondari.

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Stanslaus Choaji, akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi hiyo.

Aidha Choaji ameeleza kwamba kwa kutoa eneo la ujenzi wa Ofisi kwa ajili ya mradi huo inadhihirisha uhusiano mzuri uliopo baina ya Serikali ya Mkoa na mradi wa shule bora jambo ambalo ameeleza kwamba linaweza kuleta matunda na kufikiwa kwa malengo ya Serikali na mradi huo.

Hata hivyo Kaimu Katibu Tawala huyo ametoa pongezi kwa timu ya Mradi wa Shule bora kwa namna ambavyo wameanza kutekeleza majukumu yao mbalimbali kupitia Halmashauri za Mkoa huo.

Choaji ameahidi kwa Niaba ya Serikali ya Mkoa kushirikiana na wadau hao kufanikisha mipango waliojiwekea kumkomboa mtoto wa shule ndani ya Singida na Taifa kwa ujumla.

Mkuu wa Kitengo cha huduma ya Jamii Ubalozi wa Uingereza Getrude Mapunda, akizungumza wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa Ofisi hiyo.

Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha huduma ya Jamii Ubalozi wa Uingereza Getrude Mapunda, amesema Mradi hauanzishi vitu vipya zaidi unatekeleza mipango ya Halmashauri ili kuunganisha rasilimali fedha na rasilimali Watu kutoka Serikali na mwenye Mradi ili kuwasaidia watoto wa kitanzania.

"Mradi hauna fedha nyingi kuliko za Serikali hivyo tukichanganya fedha nyingi za Serikali na zile kidogo za Mradi tunaweza kufikia malengo ya Halmashauri zilizojiwekea katika kuboresha Elimu ya Msingi na Sekondari " alisema Getrude.

Hata hivyo ameomba ushirikiano uliopo uendelee baina ya Mkoa wa Singida na shule bora ili kufikia malengo waliyojiwekea huku akibainisha kwamba changamoto za wanafunzi mashuleni zinatofautiana kwa kila Mkoa.

Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoani Singida Samweli Daniel, akitoa taarifa wakati wa hafla ya uzinduzi huo.

Awali akitoa taarifa yake kwenye Mkutano huo Mratibu wa Mradi wa Shule Bora Mkoani Singida Samweli Daniel, amewapongeza viongozi wa Shule bora ambao wametokea Ubalozi wa Uingereza kuja kwenye uzinduzi wa Ofisi hiyo.

Amesema uwepo wa Ofisi hizo utasidia sana katika utekelezaji wa majukumu yao hasa kuhakikisha shule bora inaboresha ujifunzaji, ufundishaji, ujumuishaji na uimarishaji wa mifumo ya elimu.

Amesema kupitia Mradi huo watahakikisha changamoto hizo zinazokabili elimu mkoani hapo zinakwisha na watoto wanapata elimu Bora kwa usawa.


Wadau mbalimbali waliojitokeza kushuhudia uzinduzi rasmi wa Ofisi ya Mradi wa Shule Bora Mkoani Singida.

No comments:

Post a Comment