Monday, November 28, 2022

Serukamba afungua Kongamano la Kitaifa kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Takwimu Barani Afrika.

 

Mkuu wa Mkoa wa Singida Peter Serukamba amesema kuna umuhimu mkubwa wa matumizi ya picha za anga (satellite) katika kutathmini mashamba na mazao yanayolimwa ili kukadiria idadi ya mavuno kulingana na mwendo wa upatikanaji wa mvua, uharibifu wa mazingira na athari zake kwa kilimo.

Kauli hiyo imaetolewa leo katika Mkutano wa ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa kuhusu Maadhimisho ya siku ya Takwimu Afrika uliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Utemini uliopo katika hoteli ya KBH mjini Singida.

Serukamba amebainisha kwamba nchi za Afrika zinaweza kuboresha mifumo ya uzalishaji wa Takwimu na kuwa ya kisasa (kidijitali) ambayo itaweza kuzalisha takwimu bora na kwa wakati.

Aidha ameendelea kueleza kwamba mifumo ya ukusanyaji wa takwimu ikiboreshwa itawezesha nchi kutabiri mambo yajayo katika uzalishaji na uwekaji wa akiba ya chakula.

Hata hivyo amebainisha kwamba Mkoa wa Singida umefanya tathmini ya mahitaji ya chakula kwa kutumia takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022 ambapo mahitaji ya chakula kwa mwaka mzima ni Tani 542,175.7 ambapo Mkoa una chakula cha kutosha ambacho ni Tani 649,850 na ziada ya Tani 107,674.5.

Kauli ya Maadhimisho hayo ni kuimarisha mifumo ya kitakwimu kwa kutumia njia za kisasa katika uzalishaji na matumizi ya Takwimu za kilimo ili kuboresha sera kwa lengo la kuimarisha uvumilivu katika Kilimo, na usalama wa chakula Afrika.

Aidha amesema kauli mbiu hiyo ina elekeza utekelezaji wa mambo manne ambayo ni kuimarisha mifumo ya takwimu iwe ya kisasa, itumike katika kuboresha takwimu bora za kilimo, zitumike kuboresha sera na kuleta uhimilivu wa kilimo, Lishe na usalama wa chakula.

No comments:

Post a Comment