Friday, March 13, 2015

TANZANIA HAITAFIKIA MALENGO YA 2025 IKIWA NA ASILIMIA 42 YA WATANZANIA WALIODUMAA.




















Afisa Lishe Mkoa wa Iringa Bw. Mwita Waibe ambaye ni mwezeshaji wa kikao cha kujadili namna ya kukabiliana na tatizo la udumavu katika Mkoa wa Singida.

Tanzania haitaweza kufikia malengo ya maendeleo kwa mwaka 2025 ikiwa tatizo la udumavu halitafanyiwa jitihada za kukabiliana  nalo ili jamii iwe yenye wabunifu, wagunduzi  na afya njema.

Kwa mujibu wa utafiti wa idadi ya watu na hali ya afya ya mwaka 2010 inaonyesha kuwa asilimia 42 ya watanzania wamedumaa hali inayoisababishia gharama kubwa serikali kutibu magonjwa yanayosababishwa na udumavu, gharama ambazo zingeelekezwa kwenye shughuli nyingine za maendeleo.

Afisa Lishe Mkoa wa Iringa Mwita Waibe kutoka taasisi ya Chakula na Lishe amesema viongozi wa halmashauri za wilaya na Mikoa wanapaswa kuchukua hatua madhubuti la kutatua tazizo la udumavu ili taifa liendelee.

Waibe amesema halmashauri na sekretarieti za Mikoa  zimeagizwa kuajiri na kuwawezesha maafisa lishe ili watoe elimu kwa jamii juu ya lishe bora, pia kuunda kamati za lishe zitakazojadili hali ya lishe katika maeneo yao na kuiweka lishe kama ajenda ya kudumu katika vikao vyote muhimu.

Ameongeza kuwa udumavu unaweza kukabiliwa iwapo siku 1000 za kwanza za uhai wa mtoto zinazingatia lishe inayoshauriwa, ikiwa ni pamoja na akina mama wajawazito kuhudhuria kliniki na kupata taarifa ya namna ya kujitunza na kuwatunza watoto wao.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Aziza Mumba ameongeza kuwa upatikanaji wa chakula sio tatizo katika jamii isipokuwa elimu ya lishe bora bado haijawafikia wananchi wengi.

Mumba amesema Mkoa wa Dodoma unaongoza kwa udumavu kwa zaidi ya asilimia 50 huku ukifuatiwa na Mkoa wa Iringa na Lindi Mikoa ambayo haina ukosefu wa chakula hali ambayo inaonyesha kuwa serikali inatakiwa kuelimisha jamii.

Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Singida Aziza Mumba akizungumza katika kikao cha kujadili namna ya kukabiliana na tatizo la udumavu Mkoani Singida.



















Baadhi ya watendaji kutoka halmashauri mbalimbali Mkoani Singida wakijadili namna ya kukabiliana na tatizo la udumavu Mkoani Singida.

No comments:

Post a Comment