Tuesday, September 26, 2023

WANANCHI IKUNGI WATAKIWA KUTUNZA MIRADI YA MAENDELEO

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2023 Abdalla Shaib Kaim, ameridhishwa na usimamizi pamoja na utekelezaji wa Miradi ya Maendeleo inayotekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mkoani Singida na kuwataka wananchi kuhakikisha wanaitunza na kuilinda ili iweze kutumika kwa muda mrefu na kufikia malengo yaliyotarajiwa.

Ameyaeleza hayo tarehe 26 Septemba, 2023 alipokuwa akitembelea miradi, kukagua na kuweka jiwe la msingi katika miradi mbalimbali iliyotekelezwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kutumia fedha za ndani, wahisani na Serikali kuu.

Aidha, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka huu akiwa katika mradi wa maji ameridhishwa na mradi wa ujenzi wa Maji unaotekelezwa katika kijiji cha Matare, kata ya Unyahati Wilayani humo huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa fedha za miradi mbalimbali hasa ya kumtua mama ndoo kichwani.

Meneja wa Ruwasa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Mhandisi Hopeness Liundi, akitoa taarifa ya mradi huo wa Maji kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge Kitaifa mwaka huu, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utaweza kuwahudumia wakazi 5036 wa kijiji cha Matare Wilayani humo.

Amesema kuwa mradi huo utasaidia kuwapatia huduma endelevu pamoja na kupanua miundombinu ya maji ili wananchi waweze kuingiza maji katika majumba yao.

Mhandisi Liundi amesema faida za mradi huo utasaidia kuwezesha wananchi wa kijiji cha Matare kupata huduma ya maji safi na salama na kutosha kwa matumizi ya kawaida na ya kiuchumi, kupunguza maambukizi ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa maji safi na salama.

Hata hivyo Mhandisi Liundi amesema kuwa mpaka sasa watu 20 tayari wameisha jitokeza kwa ajili ya kuomba huduma ya kuingiziwa maji majumbani.

Katika hatua nyingine Mwenge wa Uhuru 2023 umezindua mradi wa ujenzi wa wodi ya wanaume, wanawake, watoto na jengo la kuifadhia maiti.

Akitoa taarifa ya mradi huo Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Ikungi Dk. Dorisila John amesema kuwa wanufaika wa mradi huo watakuwa wananchi, watumishi ambao watakaopata huduma bora ya afya.

Aidha Dk. Dorisila amesema kuwa mradi huo utatoa huduma bora ya afya kwa wananchi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo wapatao 426,200 na wananchi wengine watakaofika kupata huduma.

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ikungi Mashariki Mhe. Miraji Jumanne Mtaturu amewasisitiza wakazi wa Halmashauri hiyo kuhakikisha wanalinda miradi yote ambayo inatekelezwa na Serikali kwa manufaa ya wote. Aidha amesema miradi inayotekelezwa kwa sasa ni sehemu tu na kueleza kuwa bado ipo miradi mingi ya maendeleo itatekelezwa.

 















Mwisho.


No comments:

Post a Comment