Saturday, June 21, 2025

NDOTO YA SINGIDA KUWA KITUO CHA VIWANDA VYA KISASA TANZANIA KUTIM


Posted on: June 21st, 2025

Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Halima Dendego amesema kuwa Mkoa wa Singida umejipambanua kuwa kitovu cha viwanda vya kisasa nchini kupitia juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya biashara, uwekezaji, na matumizi ya rasilimali zilizopo kikamilifu. 

Akizungumza katika Mkutano wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Singida uliofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dendego amesema kuwa Mkoa wa Singida umeendelea kuongeza idadi ya viwanda hadi kufikia 1,565 huku akibainisha kuwa viwanda vikubwa vimefikia 9, vya kati 11, vidogo 420 na vidogo sana 1,225 ambavyo kwa pamoja vinazalisha ajira kwa vijana na kuongeza mzunguko wa fedha kwa wananchi.

Amesema maendeleo haya ni matokeo ya mazingira bora yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanzania inaingia katika uchumi wa viwanda kupitia uwekezaji wenye tija unaolenga kutumia rasilimali zinazopatikana katika kila mkoa. Ameongeza kuwa Mkoa wa Singida una rasilimali nyingi zikiwemo kilimo, madini, mifugo, na eneo zuri la kijiografia ambalo linaifanya Singida kuwa sehemu bora ya uwekezaji nchini.

Katika kuhakikisha kuwa viwanda hivyo vinaendelea kuzalisha kwa ufanisi, Mhe. Dendego amesema Serikali ya Mkoa imeweka mkazo mkubwa kwenye kilimo cha kisasa ambacho kinazalisha malighafi kwa ajili ya viwanda vya usindikaji. Aidha, amesema Mkoa unatarajia kuanza ujenzi wa soko la kimataifa la vitunguu kupitia mradi wa TACTIC kwa mwaka wa fedha 2025/2026, ambapo tayari mikataba imeshasainiwa.

 “Hii ni hatua kubwa ambayo itawainua wakulima wetu kwa kuwapatia soko la uhakika na kuongeza kipato chao kupitia thamani ya mazao wanayoyazalisha,” amesema Mhe.Dendego.

Kadhalika,ameongeza kuwa Serikali ya Mkoa inaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji kwa kushirikiana na taasisi kama TANESCO, TARURA, SUASA, na TANROADS katika kuhakikisha huduma za msingi kama umeme, maji, na barabara zinapatikana kwa urahisi katika maeneo yote ya Mkoa wa Singida. Amesema kuwa pamoja na fursa za kilimo, Mkoa pia una fursa kubwa katika sekta ya madini ikiwemo dhahabu, gypsum, shaba, aluminium na shaba nyeusi, na kwamba wawekezaji wanakaribishwa kuwekeza kwa wingi katika maeneo haya.

Kwa upande wake Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, akihitimisha mkutano huo, amewapongeza wajumbe wote kwa michango yao chanya iliyolenga kukuza uchumi wa mkoa. Amesema kikao hicho ni muhimu kwa kuwa uwekezaji na biashara ndiyo njia pekee ya kuzalisha fedha, siyo ajira pekee. Amewataka watumishi wa umma katika halmashauri kuwa na uelewa wa mazingira ya biashara ili kushirikiana kwa karibu na sekta binafsi katika kutengeneza mazingira rafiki ya uwekezaji.

 Dkt. Mganga amesema kuwa kikao hicho cha Baraza la Biashara kina umuhimu mkubwa kwa kuwa kinatoa majadiliano yatakayoleta maboresho ya mazingira ya biashara na uwekezaji akisema ni lazima taasisi za umma zichukue nafasi yake katika kuweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi ili kushirikiana katika uchumi. 

"Tukisikia tajiri mkubwa duniani hana ajira ya kawaida, wote ni wafanyabiashara. Biashara ndiyo njia pekee ya kuzalisha fedha. Wananchi wakizalisha fedha na sekta binafsi ikiongezeka, basi mzunguko wa fedha utaongezeka na ustawi wa jamii utaonekana," amesema.

Dkt. Mganga amesema mkoa umeweka kipaumbele katika kuhakikisha kuwa wakulima wanajiunga na vyama vya ushirika ili waweze kupata tija zaidi kwenye uzalishaji wao. Aidha, amepongeza juhudi za wakurugenzi wa halmashauri kwa kuboresha miundombinu na kuwafanya wawekezaji kuwa na mazingira rafiki ya kuwekeza huku akisisitiza kila halmashauri kutekeleza mpango wa kuwa na One Business Center ili wananchi wapate elimu ya biashara na uwekezaji kwa ukaribu zaidi.

Naye Katibu Tawala Msaidizi sehemu  ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara Bi. Donatila Vedasto ametoa taarifa ya hali ya biashara na uwekezaji katika Mkoa akisema kuwa Mkoa wa Singida una fursa nyingi sana ambazo zinahitaji kushirikiana kati ya sekta ya umma na sekta binafsi ili kuziwezesha kutumika ipasavyo.

 Amesema kuwa mpaka sasa kuna wafanyabiashara waliopo na wanaolipa kodi wapatao 10,400 waliopo kwenye makundi ya wakubwa, wa kati, na wadogo, huku machinga walioandikishwa ni 15,898. Amesema hatua hiyo inaonesha mwelekeo mzuri wa utayari wa wananchi kuingia kwenye sekta ya biashara.

Ameongeza kuwa sekta ya uwekezaji inahitaji msukumo zaidi kutoka kwa wawekezaji wa ndani hususan kwenye maeneo ya huduma kama Shopping Malls, Resting Places, na vitega uchumi vya halmashauri ili kuongeza mapato akibainisha kuwa Mkoa wa Singida umejipambanua kama mkoa tajiri wenye rasilimali nyingi za kuendeleza viwanda na biashara zenye tija kubwa kwa Taifa.

Wajumbe wa Baraza la Biashara wakiwemo kutoka sekta za madini, TRA, OSHA, COPRA na taasisi nyingine wameelezea namna Mkoa wa Singida unavyotoa fursa adhimu kupitia madini mbalimbali kama dhahabu, gypsum, aluminium, chumvi na shaba. Pia wamependekeza kuanzishwa kwa majukwaa ya pamoja baina ya wadau wa sekta binafsi na umma ili kusikiliza changamoto na kutoa mapendekezo ya pamoja yatakayowezesha maendeleo ya haraka ya sekta ya biashara.

Kikao cha Baraza la Biashara Mkoa wa Singida pia kimehimiza kuangalia upya namna bora ya kuwawezesha wakulima kupitia vyama vya ushirika ili kuondokana na dhuluma za bei na kupatikana kwa malighafi ya kutosha kwa viwanda. Aidha, kikao hicho kimeazimia kuwepo kwa ushirikiano zaidi kati ya taasisi za serikali na sekta binafsi ili kuhakikisha Mkoa wa Singida unafikia azma ya kuwa kitovu cha viwanda vya kisasa nchini.



No comments:

Post a Comment