
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Mhe. Halima Dendego, akiwa mgeni rasmi katika mikutano maalum ya Baraza la Madiwani kwa Halmashauri za Wilaya ya Ikungi na Mkalama, ametoa maagizo ya moja kwa moja kwa Wakurugenzi na Watendaji wote kuhakikisha hoja zote za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinafungwa ifikapo Julai 15, 2025, huku akipiga marufuku kuzalisha hoja mpya kwa kisingizio chochote akionya kuwa hoja mpya ni dalili ya uzembe wa moja kwa moja na ni hatari kwa ufanisi wa Serikali.
RC Dendego amesisitiza kuwa hayuko tayari kuona hoja mpya zikizaliwa kwa sababu hiyo ni sawa na kuruhusu maradhi katika mfumo wa utendaji kazi wa Serikali.
"Kwa hiyo Mkurugenzi, banana na yeyote anayezalisha hoja mpya. Tukiona hoja mpya, tunajua kuna mtu anakula bila kunawa. Huo ni uzembe, na uzembe ni kipindupindu kwenye ofisi yako,” amesema kwa lugha ya picha akiwataka viongozi wa halmashauri kuhakikisha uwajibikaji wa hali ya juu.
Kadhalika,ameelekeza kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu, kila uamuzi wa Baraza la Madiwani uliofikiwa kabla ya kuvunjwa kwa mabaraza utekelezwe kikamilifu akisisitiza kuwa utekelezaji wa maamuzi ya mabaraza ni sehemu ya heshima kwa madiwani waliomaliza muda wao, na ni msingi wa kuendeleza imani kwa wananchi.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, Dkt. Fatuma Mganga, amesema kuwa ufuatiliaji wa hoja za ukaguzi lazima ufanyike kwa maandishi na kwa nyaraka zenye ushahidi wa hatua zilizochukuliwa.
Ameongeza kuwa Halmashauri hazipaswi kutegemea vyanzo vya kawaida pekee katika mapato, bali ziendelee kubuni miradi ya kimkakati kama vile uwekezaji wa hewa ya ukaa na uanzishaji wa viwanda vidogo ili kuongeza mapato endelevu.
Aidha, Dkt. Mganga aliwakumbusha wakurugenzi na wataalamu kuwa uandaaji wa taarifa, matumizi sahihi ya mifumo ya kielektroniki na utunzaji wa kumbukumbu ni msingi wa uwajibikaji akihimiza Halmashauri kubuni vyanzo vipya vya mapato ikiwemo uwekezaji wa hewa ya ukaa, ujenzi wa viwanda vidogo na kuimarisha usimamizi wa rasilimali ardhi na mazao ya kilimo.
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Mkoa wa Singida, Bw. Othman Mwinjuma Jumbe, ameeleza kuwa kwa Halmashauri ya Mkalama, hoja nyingi zimepatiwa ufumbuzi lakini bado kuna hitaji kubwa la kuimarisha elimu kwa watendaji kuhusu namna ya kuandaa nyaraka, kufunga hoja na kuepuka hoja mpya. Kadhalika ameunga mkono hatua zinazochukuliwa na kuahidi ushirikiano wa karibu na kila halmashauri katika kusafisha na kuimarisha mifumo ya udhibiti wa fedha.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Ikungi, Mhe. Thomas Apson, amebainisha kuwa Halmashauri yake imekusanya mapato kwa zaidi ya asilimia 140 ya lengo na wameweka mikakati ya kubaini mianya ya upotevu wa mapato, hususani kwenye sekta ya kilimo na biashara huku akiahidi kuongeza msukumo katika utekelezaji wa maelekezo ya RC kwa kushirikiana na wataalamu waliopo katika kila kata.
Kadhalika Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali, amesema kuwa nidhamu ya fedha, matumizi sahihi ya sheria na usimamizi wa hoja kwa wakati ndio silaha pekee ya kulinda maendeleo ya wananchi akisisitiza kuwa Serikali haitavumilia ulegevu wowote kutoka kwa watendaji wa ngazi yoyote ile.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Ikungi, Mh. Ally Juma Mwanga, alisema kuwa kati ya hoja 26 za ukaguzi, saba zimefungwa na 19 bado ziko kwenye mchakato wa utekelezaji. Alimhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa wataendelea kusimamia utekelezaji wa maamuzi na hoja kwa karibu na kwa kasi inayotakiwa ili kufanikisha maelekezo ya Serikali.
Kadhalika,Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mkalama Mhe. James Mkwega alitoa pongezi kwa uongozi wa Mkoa kwa usimamizi madhubuti wa miradi ya maendeleo na kupendekeza kuwa uwanja wa Bombadia ubatizwe jina la Dendego, akisema Mkuu huyo wa Mkoa amekuwa mfano wa kiongozi anayetenda kwa vitendo katika kuhamasisha utekelezaji wa miradi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Ikungi, Bw. Kastory Msigala, amesema kuwa hoja zote zipo katika hatua nzuri za utekelezaji, na akatoa wito kwa Wakuu wa Idara kuhakikisha hawasubiri kukumbushwa bali wachukue hatua kwa wakati. Kadhalika ameahidi kuwa ofisi yake itafikia lengo la kufunga hoja zote ndani ya muda uliowekwa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mkalama, Bi. Asia Messos, alisema kuwa Halmashauri hiyo imeendelea kupokea hati safi kwa miaka minne mfululizo na sasa inahakikisha hoja zote zilizopo zimefungwa kupitia njia za maridhiano, ushauri wa kitaalamu na ufuatiliaji wa karibu.
Mikutano hiyo maalum ya baraza la madiwani imefanyika ikiwa ni sehemu ya hatua za mwisho kabla ya kuvunjwa kwa mabaraza yote nchini kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa serikali za mitaa. Mkoa wa Singida umeonesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kila hoja ya ukaguzi inashughulikiwa kwa matokeo, si kwa maneno pekee bali kwa ajili ya wananchi.
Kwa ujumla Mikutano hiyo maalum ya mabaraza maalum imefanyika kwa mafanikio makubwa kabla ya kuvunjwa kwa mabaraza ya madiwani nchini kote, ikiwa ni agizo kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI. Mkoa wa Singida, chini ya uongozi wa Mkuu wa Mkoa Mhe. Halima Dendego, umeonesha msimamo thabiti wa kuhakikisha hoja za ukaguzi hazibaki kama historia, bali zinapatiwa majibu na hatua, huku fedha za umma zikisimamiwa kwa tija na ufanisi kwa maendeleo ya wananchi.
No comments:
Post a Comment