Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe.Halima Dendego amewaasa waumini wa dini ya kiislamu kuhakikisha matendo mema yanakuwa sehemu ya maisha yao na wala sio kutenda mema katika kipindi cha mfungo wa Ramadhani pekee.
Ameyasema hayo wakati wa kupata ifutari pamoja na waumini wa dini ya kiislamu iliyoandaliwa Katika kuunga mkono mfungo wa mwezi mtukufu wa ramadhani katika Kiwanda cha kuchambua pamba cha Bioustain mkoani Singida, wakifuturisha waumini wa Kiislamu na wananchi wengine waliojumuika pamoja.
Akizungumza katika iftari hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Singida Mheshimiwa Halima Dendego amepongeza uongozi wa kiwanda hicho kwa kuweza kufuturisha, huku akisema kitendo hicho kinampendeza mwenyezi Mungu kwa kuonyesha ishara ya mshikamano na upendo kwa Waislamu na jamii kwa ujumla.
"Sadaka kama hizi ni jambo la heri, mwenyezi Mungu anawapenda wanaojitolea kwa ajili ya wenzao wengi, na bila shaka, huu ni mfano wa kuigwa," alisema Mheshimiwa Dendego.
Katika hatua nyingine, Mhe.Dendego, amewakumbusha Wananchi kutumia vizuri sherehe za mei mosi, zitakazofanyika kitaifa mwaka huu mkoani Singida akisema sherehe hizo ni fursa adhimu kwa wananchi wa mkoa wa Singida, kwani kwa muda wa wiki mbili mkoa utapokea zaidi ya wageni 6,000, ambao watahitaji huduma mbalimbali, ikiwemo chakula na malazi.
"Hii ni nafasi nzuri kwa wafanyabiashara na watoa huduma mbalimbali kuweza kujiandaa ipasavyo, ili wanufaike kiuchumi...tuitumie vyema fursa hii kwa kuongeza kipato chetu, na kuboresha maisha ya familia zetu," alisisitiza Dendego.
Naye Sheikh wa Mkoa wa Singida, Issah Nassoro, ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa waumini wa Kiislamu na jamii kwa ujumla, kuendelea na mwenendo mzuri hata baada ya Ramadhani.
"Tusirejee kwenye dhuluma na maovu, naomba wafanyabiashara wazingatie njia halali za kutafuta riziki, huku nao watumishi wa umma watosheke na mishahara yao, badala ya kujihusisha na vitendo vya rushwa, amesema.

Matendo mema, uadilifu na mshikamano ni nguzo muhimu si kwa mwezi wa Ramadhani pekee, bali kwa maisha ya kila siku, na ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha thamani ya mfungo wa mwezi mtukufu, inakuwa sehemu ya maisha ya kudumu.
No comments:
Post a Comment